The chat will start when you send the first message.
1Linda hatua zako uendapo katika nyumba ya Mungu. Karibia usikilize kuliko kutoa dhabihu ya wapumbavu, ambao hawajui kuwa wanafanya kosa.
2Usiwe mwepesi kuzungumza,
usiwe na haraka katika moyo wako
kuzungumza lolote mbele za Mungu.
Mungu yuko mbinguni
nawe uko duniani,
kwa hiyo maneno yako
na yawe machache.
3Kama vile ndoto huja
wakati kuna shughuli nyingi,
ndivyo yalivyo mazungumzo ya mpumbavu
wakati kuna maneno mengi.
4Unapomwekea Mungu nadhiri, usikawie kuitimiza. Yeye hafurahii wapumbavu; timiza nadhiri yako.
5Ni afadhali usiweke nadhiri kuliko kuiweka na usiitimize.
6Usiruhusu kinywa chako kukuingiza dhambini. Tena usijitetee mbele ya huyo mjumbe wa hekaluni, ukisema, “Niliweka nadhiri kwa makosa.” Kwa nini Mungu akasirike kwa ajili ya yale unayosema na kuiharibu kazi ya mikono yako?
7Kuota ndoto kwingi na maneno mengi ni ubatili. Kwa hiyo mche Mungu.
8Ukiona maskini wanaodhulumiwa katika nchi, na hukumu na haki vikipotoshwa, usishangazwe na mambo hayo; kwa maana afisa mmoja anaangaliwa na aliye juu yake, na juu ya hao wawili kuna wengine walio juu yao.
9Mafanikio ya nchi ni kwa ajili ya wote, hata mfalme mwenyewe hufaidi kutoka mashambani.
10Yeyote apendaye fedha kamwe
hatosheki na fedha;
yeyote apendaye utajiri kamwe
hatosheki na kipato chake.
Hili nalo pia ni ubatili.
11Mali ikiongezeka, ndivyo walaji
wanavyoongezeka.
Hii nayo inamfaidia nini mwenye mali
isipokuwa ni kushibisha macho yake?
12Usingizi wa kibarua ni mtamu,
awe amekula kidogo au kingi,
lakini wingi wa mali
humnyima tajiri usingizi.
13Nimeshaona uovu mzito chini ya jua:
Utajiri uliolimbikizwa
na kuleta madhara kwa mwenye mali;
14au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya,
kiasi kwamba wakati akiwa na mwana
hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake.
15Mtu hutoka tumboni mwa mama yake uchi,
naye jinsi alivyokuja vivyo hivyo huondoka.
Hachukui chochote kutokana na kazi yake
ambacho anaweza kukibeba mkononi mwake.
16Hili nalo ni baya la kusikitisha:
Kama vile mtu ajavyo, vivyo hivyo huondoka,
naye anapata faida gani,
maadamu hutaabika kwa ajili ya upepo?
17Siku zake zote hula gizani,
pamoja na fadhaa kubwa,
mateso na hasira.
18Ndipo nikatambua kwamba ni vyema na sahihi kwa mtu kula na kunywa na kutosheka katika kazi yake ngumu chini ya jua katika siku chache za maisha yake Mungu alizompa, kwa maana hili ndilo fungu lake.
19Zaidi ya yote, Mungu anapompa mtu yeyote utajiri na milki, humwezesha kuvifurahia, kukubali fungu lake na kuwa na furaha katika kazi yake, hii ni karama ya Mungu.
20Mara chache mtu huzifikiri siku za maisha yake, kwa sababu Mungu humfanya ashikwe na furaha ya moyoni.