Ezekieli 4

Ezekieli 4

Mfano wa kuzingirwa kwa Yerusalemu

1“Mwanadamu, sasa chukua tofali, uliweke mbele yako na uchore juu yake ramani ya mji wa Yerusalemu.

2Kisha uuzingire: Njenga husuru dhidi yake, na upandishe kilima hadi kuta zake, weka kambi dhidi yake pande zote, pamoja na magogo ya kubomoa.

3Kisha chukua bamba la chuma, ukalisimamishe liwe kama ukuta wa chuma kati yako na huo mji, nawe uuelekeze uso wako. Huo mji utakuwa katika hali ya kuzingirwa, nawe ndiwe utakayeuzingira. Hii itakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli.

4“Kisha ulale kwa upande wako wa kushoto na uweke dhambi za nyumba ya Israeli juu yako. Utazibeba dhambi zao kwa idadi ya siku utakazolala kwa huo upande mmoja.

5Nimekupangia idadi ya siku kama miaka ya dhambi yao. Kwa hiyo kwa siku mia tatu na tisini (390), utabeba dhambi za nyumba ya Israeli.

6“Baada ya kumaliza hili, lala chini tena, wakati huu ulale chini kwa upande wa kuume, uchukue dhambi za nyumba ya Yuda. Nimekupangia siku arobaini, siku moja kwa kila mwaka.

7Geuza uso wako uuelekeze Yerusalemu uone jinsi ulivyozingirwa, na kwa mkono wako usiovikwa nguo, tabiri dhidi yake.

8Nitakufunga kwa kamba ili usiweze kugeuka kutoka upande mmoja hadi upande mwingine, hata utakapotimiza siku za kuzingirwa kwako.

9“Chukua ngano na shayiri, maharagwe na dengu, mtama na mawele, uviweke na kuvihifadhi vyote kwenye gudulia la kuhifadhia, na uvitumie kujitengenezea mkate. Utaula mkate huo kwa hizo siku mia tatu na tisini (390) utakazokuwa umelala kwa upande mmoja.

10Pima shekeli ishirini za chakula utakachokula kwa kila siku, nawe utakula kwa wakati uliopangwa.[#4:10 Shekeli 20 ni sawa na gramu 200.]

11Pia pima maji sehemu ya sita ya hini, nawe utakunywa kwa wakati uliopangwa.[#4:11 Sehemu ya sita ya hini ni sawa na mililita (ml) 600.]

12Nawe utakula chakula vile ungekula mkate wa shayiri; uoke mkate mbele ya macho ya watu, ukitumia moto wa kinyesi cha mwanadamu.”

13Bwana akasema, “Hivi ndivyo watu wa Israeli watakavyokula chakula kilicho najisi miongoni mwa mataifa ninakowapeleka.”

14Ndipo nikasema, “Sivyo Bwana Mwenyezi! Kamwe mimi sijajitia unajisi. Tangu ujana wangu hadi sasa sijala kamwe kitu chochote kilichokufa au kilichoraruliwa na wanyama pori. Hakuna nyama yoyote najisi iliyoingia kinywani mwangu.”

15Akasema, “Vema sana, basi nitakuruhusu uoke mkate wako kwa kutumia kinyesi cha ngʼombe badala ya kinyesi cha mwanadamu.”

16Kisha Mungu akaniambia, “Mwanadamu! Mimi nitasababisha uhaba wa chakula katika Yerusalemu. Watu watakula chakula cha mgawo kwa wasiwasi, na maji ya mgawo kwa kukata tamaa,

17kwa kuwa chakula na maji vitakuwa adimu. Kila mmoja atastaajabu kumwona mwenzake, nao watadhoofika kwa sababu ya dhambi yao.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.