Wagalatia 6

Wagalatia 6

Chukulianeni mizigo

1Ndugu zangu, ikiwa mtu amepatikana akitenda dhambi, basi ninyi mnaoishi kwa Roho mnapaswa kumrejesha mtu huyo kwa upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa.

2Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

3Mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe.

4Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine.

5Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.

6Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

7Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna.

8Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

9Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.

10Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waumini.

Si kutahiriwa bali kuwa kiumbe kipya

11Angalieni herufi kubwa ninazotumia nikiwaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!

12Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo.

13Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu.

14Lakini mimi naomba nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwake ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.

15Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu!

16Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, hata kwa Israeli wa Mungu.

17Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu.

18Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.