Yohana 3

Yohana 3

Nikodemo amwendea Yesu usiku

1Basi palikuwa na mtu mmoja Farisayo, jina lake Nikodemo, mmoja wa Baraza la Wayahudi lililotawala.[#3:1 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.]

2Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.”

3Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu anayeweza kuuona ufalme wa Mungu kama hajazaliwa mara ya pili.”

4Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!”

5Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho.

6Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho.

7Kwa hiyo usishangae ninapokuambia, ‘Huna budi kuzaliwa mara ya pili.’

8Upepo huvuma kokote unakopenda. Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu unakotoka wala unakoenda. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.”

9Nikodemo akamuuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?”

10Yesu akamwambia, “Wewe ni mwalimu wa Waisraeli, nawe huelewi mambo haya?

11Amin, amin ninakuambia, sisi tunazungumza lile tunalolijua na tunashuhudia lile tuliloliona. Lakini ninyi watu hamkubali ushuhuda wetu.

12Nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamkuniamini, mtaniaminije basi nitakapowaambia mambo ya mbinguni?

13Hakuna mtu yeyote aliyeenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani Mwana wa Adamu.

14Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu,

15ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.

16“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

17Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

18Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.

19Hii ndiyo hukumu: Kwamba nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru, kwa sababu matendo yao ni maovu.

20Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe.

21Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

Ushuhuda wa Yohana Mbatizaji kuhusu Yesu

22Baada ya haya, Yesu na wanafunzi wake walienda katika eneo la Yudea, nao wakakaa huko kwa muda na kubatiza watu.

23Yohana naye alikuwa akibatiza watu huko Ainoni karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji mengi. Watu wakamjia huko ili kubatizwa.

24(Hii ilikuwa kabla Yohana hajafungwa gerezani.)

25Mashindano yakazuka kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja kuhusu suala la desturi ya kunawa kwa utakaso.

26Wakamwendea Yohana wakamwambia, “Rabi, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ngʼambo ya Yordani, yule uliyeshuhudia habari zake, sasa anabatiza na kila mtu anamwendea!”

27Yohana akawajibu, “Hakuna mtu yeyote awezaye kupata kitu chochote isipokuwa kile tu alichopewa kutoka mbinguni.

28Ninyi wenyewe ni mashahidi wangu kwamba nilisema, ‘Mimi si Kristo, ila nimetumwa nimtangulie.’[#3:28 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]

29Bibi arusi ni wa bwana arusi. Lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama karibu naye na kusikiliza kutoka kwake, hufurahi sana aisikiapo sauti ya bwana arusi. Kwa sababu hii furaha yangu imekamilika.

30Yeye hana budi kuwa mkuu zaidi na mimi nizidi kupungua.

Yeye aliyetoka mbinguni

31“Yeye ajaye kutoka juu yu juu ya yote, yeye aliye wa duniani ni wa dunia, naye huzungumza mambo ya duniani. Yeye aliyekuja kutoka mbinguni, yu juu ya yote.

32Yeye hushuhudia yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna yeyote anayekubali ushuhuda wake.

33Lakini yeyote anayekubali huo ushuhuda anathibitisha kwamba, Mungu ni kweli.

34Yeye aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, kwa kuwa Mungu humpa Roho pasipo kipimo.

35Baba anampenda Mwana, naye ametia vitu vyote mkononi mwake.

36Yeyote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.