Maombolezo 1

Maombolezo 1

1Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa,

mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu!

Jinsi umekuwa kama mama mjane,

ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa!

Yule aliyekuwa malkia miongoni mwa majimbo

sasa amekuwa mtumwa.

2Kwa uchungu, hulia sana usiku,

machozi yapo kwenye mashavu yake.

Miongoni mwa wapenzi wake wote

hakuna yeyote wa kumfariji.

Rafiki zake wote wamemsaliti,

wamekuwa adui zake.

3Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili,

Yuda ameenda uhamishoni.

Anakaa miongoni mwa mataifa,

hapati mahali pa kupumzika.

Wote ambao wanamsaka wamemkamata

katikati ya dhiki yake.

4Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza,

kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja

kwenye sikukuu zake zilizoamriwa.

Malango yake yote yamekuwa ukiwa,

makuhani wake wanalia kwa uchungu,

wanawali wake wanahuzunika,

naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu.

5Adui zake wamekuwa mabwana zake,

watesi wake wana amani.

Bwana amemletea huzuni

kwa sababu ya dhambi zake nyingi.

Watoto wake wameenda uhamishoni,

wamekuwa mateka mbele ya adui.

6Fahari zilizokuwa zake zimeondoka

kutoka kwa Binti Sayuni.

Wakuu wake wako kama ayala

ambaye hapati malisho,

wakiwa dhaifu wamekimbia

mbele ya aliyewakimbiza.

7Katika siku za mateso yake na kutangatanga,

Yerusalemu hukumbuka hazina zote

ambazo zilikuwa zake siku za kale.

Watu wake walipoanguka katika mikono ya adui,

hapatakuwa na yeyote wa kumsaidia.

Watesi wake walimtazama

na kumcheka katika maangamizi yake.

8Yerusalemu ametenda dhambi sana

kwa hiyo amekuwa najisi.

Wote waliomheshimu wanamdharau,

kwa maana wameuona uchi wake.

Yeye mwenyewe anapiga kite

na kugeukia mbali.

9Uchafu wake umegandamana na nguo zake;

hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye.

Anguko lake lilikuwa la kushangaza,

hapakuwa na yeyote wa kumfariji.

“Tazama, Ee Bwana , teso langu,

kwa maana adui ameshinda.”

10Adui ametia mikono

juu ya hazina zake zote,

aliona mataifa ya kipagani

wakiingia mahali patakatifu pake,

wale uliowakataza kuingia

kwenye kusanyiko lako.

11Watu wake wote wanalia kwa uchungu

watafutapo chakula;

wanabadilisha hazina zao kwa chakula

ili waweze kuendelea kuishi.

“Tazama, Ee Bwana , uangalie;

kwa maana nimedharauliwa.”

12“Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando?

Angalieni kote mwone.

Je, kuna maumivu kama maumivu yangu

yale yaliyotiwa juu yangu,

yale Bwana aliyoyaleta juu yangu

katika siku ya hasira yake kali?

13“Kutoka juu alipeleka moto,

akaushusha katika mifupa yangu.

Aliitandia wavu miguu yangu

na akanirudisha nyuma.

Akanifanya mkiwa,

na mdhaifu mchana kutwa.

14“Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira,

kwa mikono yake zilifumwa pamoja.

Zimefika shingoni mwangu

na Bwana ameziondoa nguvu zangu.

Amenitia mikononi mwa wale

ambao siwezi kushindana nao.

15“Bwana amewakataa mashujaa

wote walio kati yangu;

ameagiza jeshi dhidi yangu

kuwaponda vijana wangu.

Katika shinikizo lake la kukamulia zabibu

Bwana amemkanyaga Bikira Binti Yuda.

16“Hii ndiyo sababu ninalia

na macho yangu yanafurika machozi.

Hakuna yeyote aliye karibu kunifariji,

hakuna yeyote wa kuhuisha roho yangu.

Watoto wangu ni wakiwa

kwa sababu adui ameshinda.”

17Sayuni ananyoosha mikono yake,

lakini hakuna yeyote wa kumfariji.

Bwana ametoa amri kwa ajili ya Yakobo

kwamba majirani zake wawe adui zake;

Yerusalemu umekuwa

kitu najisi miongoni mwao.

18“Bwana ni mwenye haki,

hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake.

Sikilizeni, enyi mataifa yote,

tazameni maumivu yangu.

Wasichana wangu na wavulana wangu

wameenda uhamishoni.

19“Niliita washirika wangu

lakini walinisaliti.

Makuhani wangu na wazee wangu

waliangamia mjini

walipokuwa wakitafuta chakula

ili waweze kuishi.

20“Angalia, Ee Bwana , jinsi nilivyo katika dhiki!

Nina maumivu makali ndani yangu,

nami ninahangaika moyoni mwangu,

kwa kuwa nimekuwa mwasi sana.

Huko nje, upanga unaua watu,

ndani, kipo kifo tu.

21“Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu,

lakini hakuna yeyote wa kunifariji.

Adui zangu wote wamesikia kuhusu dhiki yangu,

wanafurahia lile ulilolitenda.

Naomba uilete siku uliyoitangaza

ili wawe kama mimi.

22“Uovu wao wote na uje mbele zako;

uwaadhibu vikali

kama ulivyoniadhibu

kwa sababu ya dhambi zangu zote.

Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi

na moyo wangu umedhoofika.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.