Luka 14

Luka 14

Yesu nyumbani mwa Farisayo

1Siku moja ya Sabato, Yesu alipoenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo, watu walikuwa wakimchunguza kwa makini.

2Hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili.

3Yesu akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?”

4Wakakaa kimya. Hivyo Yesu akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.

5Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ngʼombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?”

6Nao hawakuwa na la kusema.

Unyenyekevu na ukarimu

7Alipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu:

8“Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe.

9Mkifanya hivyo, yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa.

10Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule aliyekualika atakapokuona, atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote.

11Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”

12Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umepata malipo.

13Bali unapoandaa karamu, waalike maskini, vilema, viwete na vipofu,

14nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”

Mfano wa karamu kuu

(Mt 22:1‑10)

15Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Yesu, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya ufalme wa Mungu!”

16Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi.

17Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’

18“Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’

19“Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ngʼombe wa kulimia, nami ninaenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’

20“Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’

21“Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’

22“Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’

23“Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyo nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ijae.

24Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”

Gharama ya kuwa mwanafunzi

(Mt 10:37‑38)

25Umati mkubwa wa watu walikuwa wakisafiri pamoja na Yesu, naye akageuka, akawaambia,

26“Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe.

27Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

28“Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha?

29La sivyo, baada ya kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki,

30wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’

31“Au je, mfalme fulani akienda vita na mfalme mwingine, si yeye huketi chini kwanza na kufikiri: je, akiwa na jeshi la watu elfu kumi, ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu elfu ishirini?

32Ikiwa hawezi, basi yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma wajumbe na kuomba masharti ya amani.

33Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Chumvi isiyofaa

(Mt 5:13; Mk 9:50)

34“Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikiwa imepoteza ladha yake, itafanywaje ili iweze kukolea tena?

35Haifai ardhi wala kwa lundo la mbolea, bali hutupwa nje.

“Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.