The chat will start when you send the first message.
1Mpeni Bwana , enyi mashujaa,
mpeni Bwana utukufu na nguvu.
2Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;
mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.
3Sauti ya Bwana iko juu ya maji;
Mungu wa utukufu hupiga radi,
Bwana hupiga radi juu ya maji makuu.
4Sauti ya Bwana ina nguvu;
sauti ya Bwana ni tukufu.
5Sauti ya Bwana huvunja mierezi;
Bwana huvunja vipande vipande
mierezi ya Lebanoni.
6Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama,
Sirioni urukaruke kama mwana nyati.
7Sauti ya Bwana hupiga
kwa miali ya radi.
8Sauti ya Bwana hutikisa jangwa;
Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi.
9Sauti ya Bwana huzalisha ayala,
na huuacha msitu wazi.
Hekaluni mwake wote wasema,
“Utukufu!”
10Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika;
Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele.
11Bwana huwapa watu wake nguvu;
Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.