The chat will start when you send the first message.
1Nitakutukuza wewe, Ee Bwana ,
kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi,
na hukuacha adui zangu
washangilie juu yangu.
2Ee Bwana Mungu wangu, nilikuita unisaidie
na wewe umeniponya.
3Ee Bwana , umenitoa Kuzimu,[#30:3 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.]
umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.
4Mwimbieni Bwana , enyi watakatifu wake;
lisifuni jina lake takatifu.
5Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,
bali upendo wake hudumu siku zote.
Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,
lakini furaha huja asubuhi.
6Nilipofanikiwa nilisema,
“Sitatikiswa kamwe.”
7Ee Bwana , uliponijalia,
uliuimarisha mlima wangu,
lakini ulipouficha uso wako
nilifadhaika.
8Kwako wewe, Ee Bwana , niliita,
niliomba rehema kwa Bwana:
9“Kuna faida gani katika kuangamia kwangu,
katika kushuka kwangu shimoni?
Je, mavumbi yatakusifu?
Je, yatatangaza uaminifu wako?
10Ee Bwana , unisikie na kunihurumia;
Ee Bwana , uwe msaada wangu.”
11Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,
ulinivua gunia ukanivika shangwe,
12ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.
Ee Bwana Mungu wangu, nitakushukuru milele.