Zaburi 33

Zaburi 33

Zaburi 33

Ukuu na wema wa Mungu

1Mwimbieni Bwana kwa furaha, enyi wenye haki;

wanyofu wa moyo wanapaswa kumsifu.

2Msifuni Bwana kwa kinubi,

mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.

3Mwimbieni wimbo mpya;

pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe.

4Maana neno la Bwana ni haki na kweli,

ni mwaminifu kwa yote atendayo.

5Bwana hupenda uadilifu na haki;

dunia imejaa upendo wake usiokoma.

6Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa,

jeshi lao la angani likaumbwa

kwa pumzi ya kinywa chake.

7Anayakusanya maji ya bahari

kama kwenye chungu;

vilindi vya bahari

anaviweka katika ghala.

8Dunia yote na imwogope Bwana ,

watu wote wa dunia wamche.

9Kwa maana Mungu alisema, na ikawa,

aliamuru na ikasimama imara.

10Bwana huzuia mipango ya mataifa,

hupinga makusudi ya mataifa.

11Lakini mipango ya Bwana inasimama imara milele,

makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote.

12Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,

watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake.

13Bwana hutazama chini kutoka mbinguni

na kuwaona wanadamu wote;

14kutoka maskani mwake huwaangalia

wote wanaoishi duniani:

15yeye ambaye huumba mioyo yao wote,

ambaye huangalia kila kitu wanachokitenda.

16Hakuna mfalme anayeokoka kwa ukubwa wa jeshi lake;

hakuna shujaa anayeokoka kwa wingi wa nguvu zake.

17Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu,

licha ya nguvu zake nyingi, hawezi kuokoa.

18Lakini macho ya Bwana yako kwa wale wamchao,

kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo,

19ili awaokoe na mauti,

na kuwahifadhi wakati wa njaa.

20Sisi tunamngojea Bwana kwa matumaini,

yeye ni msaada wetu na ngao yetu.

21Mioyo yetu humshangilia,

kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu.

22Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Bwana ,

tunapoliweka tumaini letu kwako.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.