The chat will start when you send the first message.
1Ee Bwana , tegea sikio maneno yangu,
uangalie kupiga kite kwangu.
2Sikiliza kilio changu ili unisaidie,
Mfalme wangu na Mungu wangu,
kwa maana kwako ninaomba.
3Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Bwana ;
asubuhi naleta haja zangu mbele zako,
na kusubiri kwa matumaini.
4Wewe si Mungu unayefurahia uovu,
kwako mtu mwovu hataishi.
5Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,
unawachukia wote watendao mabaya.
6Unawaangamiza wasemao uongo.
Bwana huwachukia
wanaomwaga damu na wadanganyifu.
7Lakini mimi, kwa rehema zako kuu,
nitakuja katika nyumba yako,
kwa unyenyekevu, nitasujudu
kulielekea Hekalu lako takatifu.
8Niongoze katika haki yako, Ee Bwana ,
kwa sababu ya adui zangu,
nyoosha njia yako mbele yangu.
9Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika,
mioyo yao imejaa maangamizi.
Koo lao ni kaburi lililo wazi,
kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu.
10Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu!
Hila zao ziwe anguko lao wenyewe.
Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi,
kwa kuwa wamekuasi wewe.
11Lakini wote wanaokimbilia kwako na wafurahi,
waimbe kwa shangwe daima.
Ueneze ulinzi wako juu yao,
ili wale wanaolipenda jina lako
wapate kukushangilia.
12Kwa hakika, Ee Bwana , unawabariki wenye haki,
unawazunguka kwa wema wako kama ngao.