Zaburi 83

Zaburi 83

Zaburi 83

Maombi kwa ajili ya kushindwa kwa adui za Israeli

1Ee Mungu, usikae kimya,

usinyamaze, Ee Mungu, usikae mbali.

2Tazama watesi wako wanafanya fujo,

jinsi adui zako wanavyoinua vichwa vyao.

3Kwa ujanja, wanapanga njama dhidi ya watu wako;

wanapanga hila dhidi ya wale unaowapenda.

4Wanasema, “Njooni, tuwaangamize kama taifa,

ili jina la Israeli lisikumbukwe tena.”

5Kwa nia moja wanapanga njama pamoja,

wanafanya muungano dhidi yako,

6mahema ya Edomu na Waishmaeli,

ya Wamoabu na Wahagari,

7Gebali, Amoni na Amaleki,[#83:7 yaani Bubilo]

Ufilisti, pamoja na watu wa Tiro.

8Hata Ashuru wameungana nao

kuwapa nguvu wazao wa Lutu.

9Uwatendee kama vile ulivyowatendea Midiani,

na kama vile ulivyowatendea Sisera na Yabini

hapo kijito cha Kishoni,

10ambao waliangamia huko Endori

na wakawa kama kinyesi juu ya ardhi.

11Wafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu,

watawala wao kama Zeba na Salmuna,

12ambao walisema, “Na tumiliki maeneo

ya malisho ya Mungu.”

13Ee Mungu wangu, wapeperushe kama mavumbi ya kisulisuli,

kama makapi yapeperushwayo na upepo.

14Kama vile moto unavyoteketeza msitu

au mwali wa moto unavyounguza milima,

15wafuatilie kwa tufani yako

na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.

16Funika nyuso zao kwa aibu

ili watu walitafute jina lako, Ee Bwana .

17Wao na waaibishwe na kufadhaishwa milele,

na waangamie kwa aibu.

18Hebu wajue kuwa wewe, ambaye jina lako ni Bwana ,

kwamba wewe peke yako ndiwe Uliye Juu Sana ya dunia yote.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.