The chat will start when you send the first message.
1Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha;
tumfanyie kelele za shangwe
Mwamba wa wokovu wetu.
2Tuje mbele zake kwa shukrani,
tumtukuze kwa vinanda na nyimbo.
3Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,
mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4Mkononi mwake mna vilindi vya dunia,
na vilele vya milima ni mali yake.
5Bahari ni yake, kwani ndiye aliyeifanya,
na mikono yake iliumba nchi kavu.
6Njooni, tusujudu, tumwabudu,
tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu,
7kwa maana yeye ndiye Mungu wetu,
na sisi ni watu wa malisho yake,
kondoo chini ya utunzaji wake.
Mkiisikia sauti yake leo,
8msiifanye mioyo yenu migumu
kama mlivyofanya kule Meriba,
kama mlivyofanya siku ile
kule Masa jangwani,
9ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima,
ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu.
10Kwa miaka arobaini nilikasirikia kizazi kile,
nikasema, “Hawa ni taifa ambalo mioyo yao imepotoka,
nao hawajazijua njia zangu.”
11Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,
“Kamwe hawataingia rahani mwangu.”