The chat will start when you send the first message.
1Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili?
2Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu.
3Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”[#4:3 Mwa 15:6]
4Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili.
5Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki.
6Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena kuhusu baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:
7“Wamebarikiwa wale
ambao wamesamehewa makosa yao,
ambao dhambi zao zimefunikwa.
8Heri mtu yule
Bwana hamhesabii dhambi zake.”
9Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tumesema imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.
10Je, ilihesabiwaje kwake kuwa haki? Ni kabla ya kutahiriwa, au baada yake kutahiriwa? Haikuwa baada yake kutahiriwa, bali kabla hajatahiriwa!
11Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote waaminio pasipo kutahiriwa, ili wahesabiwe kuwa wenye haki.
12Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.
13Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kupitia kwa sheria bali kupitia kwa haki ipatikanayo kwa imani.
14Kwa maana ikiwa wale wanaoishi kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu,
15kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria, hakuna makosa.
16Kwa hiyo, ahadi huja kupitia kwa imani, ili iwe ni kwa neema, na ihakikishiwe wazao wote wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote.
17Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anayefufua waliokufa, na kuvitaja vitu ambavyo haviko kana kwamba viko.[#4:17 Mwa 17:5]
18Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”[#4:18 Mwa 15:5]
19Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri hali ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri hali ya kufa ya tumbo la Sara.
20Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu,
21akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi.
22Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.”[#4:22 Mwa 15:6]
23Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake,
24bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupatia haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu.
25Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.