The chat will start when you send the first message.
1Boazi akakwea hadi lango la mji, akaketi pale. Yule mtu wa jamaa aliyekuwa wa karibu wa kukomboa, ambaye Boazi alimtaja, akaja. Boazi akasema, “Njoo hapa, rafiki yangu. Karibu uketi.” Naye akakaribia, akaketi.
2Boazi akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, “Ketini hapa.” Nao wakaketi.
3Kisha akamwambia yule jamaa wa karibu wa kukomboa, “Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi iliyokuwa mali ya ndugu yetu Elimeleki.
4Nami niliwaza nikujulishe wewe na kukuambia uinunue mbele ya hawa waliopo hapa, na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya fanya hivyo. Lakini kama hutaikomboa, uniambie, ili nijue. Kwa kuwa hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuikomboa ila wewe na baada yako ni mimi.”
Naye akasema, “Nitaikomboa mimi.”
5Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua hiyo ardhi kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabu, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.”
6Aliposikia hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kuikomboa, kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe ikomboe mwenyewe. Mimi sitaweza.”
7(Basi katika siku za kale huko Israeli, ili kukamilisha tendo la kukomboa na kukabidhiana mali, mmoja huvua kiatu chake na kumpatia mwingine. Hii ilikuwa ni njia ya kuhalalisha mabadilishano katika Israeli.)
8Basi yule jamaa wa karibu wa kukomboa akamwambia Boazi, “Wewe inunue mwenyewe.” Naye huyo jamaa akavua kiatu chake.
9Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni.
10Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabu, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali yake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake, wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!”
11Kisha wazee pamoja na watu wote waliokuwa langoni wakasema, “Sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wanawake wawili ambao pamoja waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata na uwe mashuhuri katika Bethlehemu.
12Kupitia kwa uzao ambao Bwana atakupa kutokana na huyu mwanamwali, jamaa yako na ifanane na ya Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda.”
13Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake. Alipoingia kwake, Bwana akamjalia Ruthu, naye akapata mimba, akamzaa mtoto wa kiume.
14Wanawake wakamwambia Naomi: “Ahimidiwe Bwana , asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote!
15Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda, na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye alimzaa.”
16Basi Naomi akamchukua yule mtoto, akampakata na akawa mlezi wake.
17Wanawake waliokuwa jirani zake wakasema, “Naomi ana mtoto wa kiume.” Wakamwita jina Obedi. Yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi.
Peresi alimzaa Hesroni,
19Hesroni akamzaa Ramu,
Ramu akamzaa Aminadabu,
20Aminadabu akamzaa Nashoni,
Nashoni akamzaa Salmoni,
21Salmoni akamzaa Boazi,
Boazi akamzaa Obedi,
22Obedi akamzaa Yese,
na Yese akamzaa Daudi.