The chat will start when you send the first message.
1Mwombeni Bwana mvua wakati wa vuli;
ndiye Bwana atengenezaye mawingu ya tufani.
Huwapa watu manyunyu ya mvua,
pia mimea ya shambani kwa ajili ya kila mtu.
2Sanamu huzungumza udanganyifu,
waaguzi huona maono ya uongo;
husimulia ndoto ambazo si za kweli,
wanatoa faraja batili.
Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo
walioteseka kwa kukosa mchungaji.
3“Hasira yangu inawaka dhidi ya wachungaji,
nami nitawaadhibu viongozi;
kwa kuwa Bwana wa majeshi
atalichunga kundi lake,
nyumba ya Yuda,
naye atawafanya kama farasi
mwenye kiburi akiwa vitani.
4Kutoka Yuda litatokea Jiwe la pembeni,
kutoka kwake vitatoka vigingi vya hema,
kutoka kwake utatoka upinde wa vita,
kutoka kwake atatoka kila mtawala.
5Kwa pamoja watakuwa kama mashujaa
wanaokanyaga barabara za matope
wakati wa vita.
Kwa sababu Bwana yu pamoja nao,
watapigana na kuwashinda wapanda farasi.
6“Nitaiimarisha nyumba ya Yuda
na kuiokoa nyumba ya Yusufu.
Nitawarejesha kwa sababu
nina huruma juu yao.
Watakuwa kama watu ambao
sijawahi kuwakataa
kwa sababu mimi ndimi Bwana Mungu wao,
nami nitawajibu.
7Waefraimu watakuwa kama mashujaa,
mioyo yao itafurahi kana kwamba ni kwa divai.
Watoto wao wataona na kufurahi,
mioyo yao itashangilia katika Bwana .
8Nitawaashiria na kuwakusanya ndani.
Hakika nitawakomboa,
nao watakuwa wengi
kama walivyokuwa mwanzoni.
9Ijapokuwa niliwatawanya miongoni mwa mataifa,
hata hivyo wakiwa katika nchi za mbali
watanikumbuka mimi.
Wao na watoto wao watanusurika katika hatari
nao watarudi.
10Nitawarudisha kutoka Misri
na kuwakusanya toka Ashuru.
Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni,
na hapo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha.
11Watapita katika bahari ya mateso;
bahari iliyochafuka itatulizwa
na vilindi vyote vya Mto Naili vitakauka.
Kiburi cha Ashuru kitashushwa,
nayo fimbo ya utawala ya Misri itatoweka.
12Nitawaimarisha katika Bwana ,
na katika jina lake watatembea,”
asema Bwana .