Zekaria 2

Zekaria 2

Maono ya tatu: Mtu mwenye kamba ya kupimia

1Kisha nikatazama juu: pale mbele yangu palikuwa na mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake!

2Nikamuuliza, “Unaenda wapi?”

Akanijibu, “Kupima Yerusalemu, kupata urefu na upana wake.”

3Kisha malaika aliyekuwa akizungumza nami akaondoka, malaika mwingine akaja kukutana naye

4na kumwambia: “Kimbia, umwambie yule kijana, ‘Yerusalemu utakuwa mji usio na kuta kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo.

5Mimi mwenyewe nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka,’ asema Bwana , ‘nami nitakuwa utukufu wake ndani yake.’

6“Njooni! Njooni! Kimbieni mtoke katika nchi ya kaskazini,” asema Bwana , “kwa kuwa nimewatawanya kwenye pande nne za mbingu,” asema Bwana .

7“Njoo, ee Sayuni! Kimbia, wewe ukaaye ndani ya Binti Babeli!”

8Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana wa majeshi: “Baada ya yeye kuniheshimu na kunituma mimi dhidi ya mataifa yaliyokuteka nyara, kwa kuwa yeyote awagusaye ninyi, anaigusa mboni ya jicho lake,

9hakika nitauinua mkono wangu dhidi yao ili watumwa wao wawateke nyara. Ndipo mtajua kuwa Bwana wa majeshi amenituma.

10“Shangilia na ufurahie, ee Binti Sayuni, kwa maana ninakuja, nami nitaishi miongoni mwenu,” asema Bwana .

11“Mataifa mengi yataunganishwa na Bwana siku hiyo, nao watakuwa watu wangu. Nitaishi miongoni mwenu, nanyi mtajua kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu.

12Bwana atairithi Yuda kama fungu lake katika nchi takatifu na atachagua tena Yerusalemu.

13Tulieni mbele za Bwana , enyi watu wote, kwa sababu ameinuka kutoka makao yake matakatifu.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.