The chat will start when you send the first message.
1Kisha akanionesha Yoshua, kuhani mkuu, akiwa amesimama mbele ya malaika wa Bwana , naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshtaki.[#3:1 Kwa Kiebrania ni Yeshua , maana yake Yehova ni wokovu.]
2Bwana akamwambia Shetani, “Bwana akukemee Shetani! Bwana , ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?”
3Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika.
4Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.”
Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.”
5Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa Bwana akiwa amesimama karibu.
6Malaika wa Bwana akamwamuru Yoshua:
7“Hivi ndivyo asemavyo Bwana wa majeshi: ‘Ikiwa utatembea katika njia zangu na kushika maagizo yangu, basi utaitawala nyumba yangu na kuzilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi miongoni mwa hawa wasimamao hapa.
8“ ‘Sikiliza, ee Yoshua kuhani mkuu, pamoja na wenzako walioketi mbele yako, ambao ni watu walio ishara ya mambo yatakayokuja: Ninaenda kumleta mtumishi wangu, Tawi.
9Tazama, jiwe nililoliweka mbele ya Yoshua! Kuna macho saba juu ya jiwe lile moja, nami nitachora maandishi juu yake,’ asema Bwana wa majeshi, ‘nami nitaiondoa dhambi ya nchi hii kwa siku moja.
10“ ‘Katika siku hiyo kila mmoja wenu atamwalika jirani yake akae chini ya mzabibu wake na mtini wake,’ asema Bwana wa majeshi.”