The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa pili wa utawala wa Artashasta, mfalme mkuu, siku ya kwanza ya mwezi wa Nisani, Mordekai, mwana wa Yairo, mwana wa Semaya, mwana wa Kiseo, wa kabila ya Benyamini, aliota ndoto.[#2 Fal 24:10-16]
2Huyu Mordekai alikuwa Myahudi akikaa katika mji wa Susa, mtu mkuu, mtumishi katika behewa la mfalme.
3Alikuwa amechukuliwa mateka, wakati Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alipomhamisha Yekonia, mfalme wa Uyahudi, kutoka Yerusalemu.
4Nayo ndoto yake ilikuwa hivi: Tazama! Kelele na ghasia; ngurumo na tetemeko la ardhi; msukosuko juu ya dunia.
5Na tazama! Kumetokea majoka makubwa mawili, wote wawili tayari kupigana.
6Mlio wao ulikuwa mkubwa mno, hata kwa kusikia tu mataifa yote walijipanga tayari kwa vita ili kupigana na taifa lenye haki.
7Na tazama! Siku ya giza na weusi; dhiki na taabu; misiba na wasiwasi mwingi juu ya dunia.
8Taifa zima la wenye haki wakafadhaika kwa kuogopa mabaya yanayowajia, wakajiweka tayari kufa. Wakamlilia Mungu,
9hata katika kilio chao, kama katika chemchemi ndogo, kulitokea mto mkubwa, maji mengi sana.
10Nuru ikaangaza, na jua likachomoza; wanyonge wakakwezwa wakawameza wenye fahari.
11Naye Mordekai alipokwisha kuiota ndoto hiyo ya mambo yaliyokusudiwa na Mungu aliamka; akaihifadhi moyoni mwake, akaitafakari maana yake hata usiku.
12Basi, Mordekai alikuwa akipumzika behewani, kama kawaida yake, pamoja na Gabatha na Thara, matowashi wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa behewa.
13Akasikia mazungumzo yao, akayapeleleza mashauri yao, akapata kufahamu ya kuwa wamejiweka tayari kumshika mfalme Artashasta. Akamwarifu mfalme habari zao.
14Mfalme akawahoji wale matowashi wawili, nao wakakiri, wakapelekwa kuuawa.
15Mfalme akayaandika mambo hayo kuwa ukumbusho, naye Mordekai pia aliandika habari zake.
16Mfalme akamwagiza Mordekai atumike behewani, akamtunukia kwa kazi zake.
17Ikawa Hamani mwana wa Hamedatha, Mbugaya, mtu mwenye heshima kuu kwa mfalme alikuwa ikiwatafuta mabaya Mordekai na watu wake kwa sababu ya hao matowashi wawili wa mfalme.