Yohana 8

Yohana 8

Mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi

1Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka katika mlima wa Mizeituni.[#Lk 21:37]

2Asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha.

3Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati.

4Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini.

5Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake kama hawa; nawe wasemaje?[#Law 20:10; Kum 22:22-24; Mt 22:15]

6Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika ardhi.

7Nao walipozidi kumhoji, aliinuka, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.[#Kum 17:7]

8Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika ardhi.

9Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.[#Mt 22:22; Rum 2:22]

10Yesu akainuka asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?

11Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; wala usitende dhambi tena.][#Yn 5:14]

Yesu nuru ya ulimwengu

12Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.[#Mt 5:14; Yn 9:5; Isa 49:6; Yn 1:5,9; 12:46]

13Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.[#Yn 5:31]

14Yesu akajibu, akawaambia, Mimi ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako.[#Yn 5:31]

15Ninyi mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu.[#Yn 7:24; 12:47]

16Nami nijapohukumu, hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi na yeye aliyenituma.[#Yn 8:29]

17Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli.[#Kum 17:6; 19:15]

18Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma ananishuhudia.[#1 Yoh 5:9]

19Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui; kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba yangu.[#Yn 14:7]

20Maneno hayo aliyasema alipokuwa akifundisha hekaluni, katika chumba cha hazina; wala hakuna mtu aliyemkamata, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.[#Yn 7:30; 13:1; Lk 22:53]

Yesu atabiri kuhusu kifo chake

21Basi akawaambia tena, Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamuwezi kuja.[#Yn 7:34; 13:33]

22Basi Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa asema, Mimi niendako ninyi hamuwezi kuja?[#Yn 7:35]

23Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.[#Yn 3:31]

24Kwa hiyo niliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.

25Basi wakamwambia, U nani wewe? Yesu akawaambia, Hasa neno lilo hilo ninalowaambia.[#Yn 8:14]

26Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenituma ni kweli, nami niliyoyasikia kwake, ndiyo ninenayo katika ulimwengu.[#Yn 8:38; 12:49]

27Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba.

28Basi Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo.[#Yn 3:14; 12:32]

29Naye aliyenituma yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo.[#Yn 8:16; Mt 27:46]

30Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamini.[#Yn 7:31; 10:42; 12:11]

Wanafunzi wa kweli

31Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli;

32tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.

33Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Abrahamu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wowote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?[#Mt 3:9; Lk 3:8; Neh 9:36]

34Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.[#Rum 6:16,20; 1 Yoh 3:8]

35Wala mtumwa hakai nyumbani siku zote; mwana hukaa siku zote.[#Gal 4:30]

36Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.[#Rum 6:18,22]

37Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Abrahamu lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu.

38Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo.

Yesu na Abrahamu

39Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Abrahamu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngezitenda kazi zake Abrahamu.[#Mt 3:9]

40Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Abrahamu hakufanya hivyo.

41Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu.[#Mwa 3:15; Kum 23:2]

42Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nilitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.[#1 Yoh 5:1]

43Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamuwezi kulisikia neno langu.[#Yn 12:39; Mt 12:34; Rum 8:7]

44Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa uongo.[#1 Yoh 3:8-10; Mwa 3:4; 2 Pet 2:4; #8:44 Kigiriki ni ‘wa huo’.]

45Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki.[#Lk 22:67]

46Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki?[#2 Kor 5:21; 1 Pet 2:22]

47Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu.[#Yn 18:37; 1 Yoh 4:6]

48Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Je! Sisi hatusemi vema ya kwamba wewe u Msamaria, nawe una pepo?[#Yn 7:20; Mk 3:21]

49Yesu akajibu, Mimi sina pepo; lakini mimi namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima yangu.

50Wala mimi siutafuti utukufu wangu; kuna yule autafutaye na ndiye hakimu.[#Yn 5:41]

51Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele.[#Yn 5:24; 6:40,47; 11:25]

52Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng'amua ya kuwa una pepo. Abrahamu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele.[#Mk 9:1]

53Wewe u mkuu kuliko baba yetu Abrahamu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani?[#Yn 4:12]

54Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu.

55Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nalishika.[#Yn 7:28]

56Abrahamu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi.

57Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Abrahamu?

58Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Kabla ya Abrahamu kuwako, mimi niko.

59Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.[#Yn 10:31]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania