Tobiti 13

Tobiti 13

Tobiti amshukuru Mungu

1Basi Tobiti akatunga sala ya kushangilia, akisema,

Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Na ufalme wake umebarikiwa.

2Kwa maana hurudi, na kurehemu tena;

Hushusha hata kuzimu, na kuinua tena;

Wala hakuna awezaye kujiepusha na mkono wake.

3Enyi wana wa Israeli, mshukuruni mbele ya mataifa

Yeye ambaye ametutawanya katikati yao.

4Huko huko utangazeni ukuu wake;[#Isa 63:16; Yer 3:4; Hek 14:3; Sira 23:1,4; Mt 6:9]

Mwadhimisheni mbele ya wote walio hai;

Kwa kuwa Yeye ndiye BWANA wetu.

Naye Mungu yu Baba yetu milele.

5Ataturudi kwa ajili ya maovu yetu,

Na kutuonesha rehema zake tena.

Atatukusanya kutoka kwa mataifa yote

Ambao tumetawanyika katikati yao.

6Mkimgeukia kwa moyo wote na roho yote

Na kutenda kweli mbele zake

Ndipo atakapowageukia ninyi,

Wala hatawaficheni uso wake.

Angalieni atakavyowatendea;

Mshukuruni kwa vinywa vyenu vyote;

Mhimidini BWANA mwenye haki:

Mkuzeni Mfalme wa milele.

Katika nchi ya kufungwa kwangu namshukuru;

Nawahubiri taifa la wakosaji nguvu zake na enzi yake.

Enyi wakosaji, geukeni, mkatende haki mbele zake;

Nani ajuaye kama atawakubali na kuwarehemu?

7Mimi namwadhimisha Mungu wangu;

Na roho yangu yamkuza Mfalme wa mbinguni:

8Naam, nitaushangilia ukuu wake.

Watu wote wamtolee shukrani katika Yerusalemu.

9Ee Yerusalemu! Ulio Mji Mtakatifu![#Isa 60:1-22; Ufu 21:9–22:5]

Atakurudi kwa ajili ya matendo ya wanao;

Tena atawarehemu watoto wa wenye haki.

10Mshukuruni BWANA kwa utauwa:

Mhimidini Mfalme wa milele.

Maskani yake ijengwe tena ndani yako kwa furaha,

Ili awafurahishe ndani yako walio wafungwa.

Na kuwapenda daima ndani yako walio na huzuni.

11Mataifa mengi watakuja kutoka mbali,

Hata kulijia jina la BWANA Mungu.

Wenye tunu mikononi mwao,

Naam, tunu kwa Mfalme wa mbinguni.

Vizazi vya vizazi watakusifu,

Na kukuimbia nyimbo za furaha.

12Wamelaaniwa wote wakuchukiao,

watabarikiwa milele wote wakupendao;

13Furahi, na kuwashangilia watoto wa wenye haki.

Kwa maana watakusanywa pamoja

Na kumhimidi BWANA wa wenye haki.

14Wa heri wote wakupendao,

Watafurahiwa kwa ajili ya amani yako.

Wa heri walioyahuzunikia mapigo yako,

Kwa sababu watakufurahia.

Wakati watakapoiona fahari yako yote,

Wakafurahishwa wenyewe hata milele.

15Roho yangu imhimidi Mungu, Mfalme mkuu,

16Kwa kuwa Yerusalemu utajengwa tena,

Kwa yakuti na zumaridi na vito vya thamani;

Kuta zake na minara na maboma kwa dhahabu safi.

Na njia za Yerusalemu zitatiwa sakafu ya mawe,

Kwa berilo na johari na vito vya Ofiri.

17Njia zake zote zitasema, Haleluya, na kumhimidi,

Kusema, Ahimidiwe Mungu aliyekukuza milele.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania