Sira 1

Sira 1

Sifa kwa Hekima

1Hekima yote hutoka kwa Bwana,

nayo imo kwake hata milele.

2Nani awezaye kuuhesabu mchanga wa pwani

au matone ya mvua?

Nani awezaye kuzihesabu siku za milele?

3Je, kimo cha mbingu ni kiasi gani?

Je, upana wa dunia ni kiasi gani?

Je, kina cha bahari ni kiasi gani?

Nani aujuaye umaarufu wa Hekima?

Nani awezaye kuyajibu maswali haya?

4Hekima iliumbwa kabla ya vitu vyote,

busara ilikuwako tangu zama zote. [

5Chanzo cha hekima ni neno la Mungu aliye juu; njia zake ni amri za milele.]

6Nani aliyeoneshwa kitovu cha Hekima?

Nani anafahamu mafumbo ya Hekima? [

7Ujuzi wa hekima alijulishwa nani? Na uzoefu wake mwingi nani aliyepata kuuelewa?]

8Yuko mmoja tu mwenye hekima wa kutisha sana,

ameketi katika kiti chake cha enzi - ndiye Bwana.

9Bwana mwenyewe ndiye aliyemuumba Hekima;

yeye ndiye aliyemwona na kumpima,

na kumjaza katika kazi zake zote.

10Hekima yumo katika kila kiumbe kadiri atoavyo Mungu;

Mungu humgawia kila mtu ampendaye.

11Kumcha Bwana huleta fahari na sifa,

huleta furaha na taji ya shangwe.

12Kumcha Bwana kwaufurahisha moyo,

kwaleta shangwe, furaha na maisha marefu.

13Amchaye Bwana atafanikiwa mwisho wake;

siku ya kufa kwake atabarikiwa.

14Kumcha Bwana ni mwanzo wa Hekima,

Hekima ameumbwa na waaminifu tangu tumboni mwa mama.

15Amejiwekea msingi wa kudumu kati ya watu,

na vizazi vijavyo vitamtegemea Hekima.

16Kumcha Bwana ni ukamilifu wa hekima,

Hekima huwatosheleza watu kwa matunda yake.

17Huzijaza nyumba zao bidhaa zote wanazohitaji

na bohari zao mazao yake.

18Kumcha Bwana ni kuvikwa taji la hekima,

Hekima huleta amani na afya nzuri.

19Bwana alimwona na kumpima,

alinyesha duniani maarifa na utambuzi,

na kuwapa fahari wale wanaomshikilia.

20Kumcha Bwana ni kitovu cha Hekima,

na matawi yake ni maisha marefu. [

21Kumheshimu Bwana huondoa dhambi; panapopatikana uchaji wa Bwana, huondosha hasira.]

22Hasira isiyo halali haikubaliki,

maana hasira husababisha maangamizi ya mtu.

23Mvumilivu husubiri hadi wakati ufaao,

na hatimaye furaha itambubujikia.

24Huyo huzuia maneno yake hadi wakati ufaao,

ndipo watu wengi wataisifu busara yake.

25Bohari za Hekima zimejaa misemo ya busara,

lakini uchaji ni chukizo kwa mwenye dhambi.

26Ukitaka hekima zishike amri,

naye Bwana atakupa hekima,

27Maana kumcha Bwana ni hekima na nidhamu,

naye hupendezwa na uaminifu na upole.

28Usitupilie mbali kumcha Bwana,

wala usimwendee kwa moyo mdanganyifu.

29Usiwe mnafiki mbele ya watu;

uuchunge mdomo wako.

30Usijitukuze, la sivyo utaanguka

na kujiletea aibu wewe mwenyewe.

Bwana atazifunua siri zako

na kukuangusha mbele ya jumuiya,

kwa kuwa hukumwendea Bwana kwa uchaji,

na moyo wako ulikuwa umejaa udanganyifu.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania