Sira 19

Sira 19

1Mfanyakazi mlevi hatakuwa tajiri.

Anayepuuza mambo madogo ataanguka kidogokidogo.

2Pombe na wanawake huwapotosha wanaume wenye akili;

mwanamume afanyaye urafiki na malaya ni mpotovu kabisa.

3Huyo mwisho wake ni kuoza na kuliwa na wadudu;

maisha yake ya uzembe yataondolewa.

4Anayewatumainia wengine haraka mno, hana akili.

Na atendaye dhambi, anajidhuru mwenyewe.

5Anayefurahia uovu, atahukumiwa.[#19:5 Hati nyingine: Moyo.; #19:5 hati nyingine huongeza: Lakini anayekataa anasa, ni mtu ayavikaye maisha yake taji. 6 Anayeutawala ulimi wake, ataishi bila ugomvi.]

Kupiga domo kaya

6Anayechukia domo kaya, anajiepusha na uovu.

7Usirudie kitu ulichoambiwa,

nawe hutapata madhara yoyote.

8Usimwambie mtu awe rafiki au adui,

isipokuwa tu kama ni dhambi kwako kunyamaza.

9Maana huenda fulani alikusikia na kukuona,

na wakati ukitimia, atakuchukia.

10Je, umewahi kusikia kitu? Na kife pamoja nawe.

Lakini usiogope! Hilo halitakupasua!

11Mpumbavu anayejaribu kuficha neno lolote,

atasikia machungu kama mama anayejifungua.

12Kama vile mshale uliompenya mtu pajani

ndivyo ilivyo neno ndani yake mpumbavu.

13Ukisikia rafiki amefanya kosa, mwulize.

Huenda si kweli; na kama ni kweli, hatarudia.

14Mwulize jirani; labda hakusema.

Na kama alisema, hatasema tena.

15Mwulize rafiki uliyoyasikia, labda hakuyasema.

Kwa hiyo usiamini kila kitu unachosikia.

16Maana mtu aweza akakosea bila kukusudia.

Nani ambaye hajawahi kukosa kwa ulimi wake?

17Ukisikia kitu juu ya jirani; mwulize, usimtishe!

Ipe nafasi sheria ya Mungu Mkuu ifanye kazi. [Na usiwe na hasira.

18Kumcha Bwana ni mwanzo wa kukubaliwa naye, na kuwa na hekima kunakufanya akupende.

19Kuzijua amri za Bwana kunaleta maisha yenye nidhamu; na wale wanaompendeza watafurahia matunda ya mti wa uzima.]

Hekima ya kweli

20Hekima yote ni kumcha Bwana;

21na hekima yote yahusu kutii sheria. [Kujua Bwana ni mwenye enzi kuu.

Mtumishi anapomwambia Bwana wake,

“Sitafanya unalotaka,”

hata kama atafanya baadaye,

anamkasirisha huyo bwana anayemtegemeza.]

22Lakini kujua uovu si hekima,

mashauri ya wenye dhambi sio busara.

23Uko ujanja ambao ni chukizo tupu.

Lakini yuko mpumbavu ambaye hana tu hekima.

24Afadhali mtu mcha Mungu asiye na akili

kuliko mtu mwerevu sana ambaye anavunja sheria.

25Kuna walio wajanja sana na hawatendi mambo ya haki;

wako na wengine wanaopotosha wema kupata haki zake.

26Wako watu walaghai wanaojidai wana huzuni,

lakini ndani wamejaa udanganyifu mtupu.

27Hao huficha nyuso zao na kujidai hawasikii;

lakini kama hawaonekani watakuangamiza.

28Na kama hawana nguvu ya kutenda dhambi,

watakapopata nafasi, wataitenda tu.

29Mtu hujulikana kwa namna anavyoonekana,

na mwenye busara utamtambua ukikutana naye.

30Mtu alivyovaa, anavyocheka na kutembea,

vyote vinamwonesha jinsi alivyo.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania