Sira 27

Sira 27

1Watu wengi wametenda dhambi kutafuta faida;

anayetaka kuwa tajiri yampasa kuchunga macho yake.

2Kama vile kigingi kilivyoshikiwa imara katika mawe ya nyumba,

ndivyo dhambi ilivyoshikiwa imara katika kuuza na kununua.

3Mtu yeyote asiyezingatia kumcha Bwana,

nyumba yake itaangamizwa punde si punde.

Hotuba

4Ukitikisa chekecheke makapi hubaki,

ndivyo na uchafu wa mtu unavyobaki katika mawazo yake.

5Tanuri hupima kazi za mfinyanzi,

ndivyo pia mazungumzo yanavyompima mtu.

6Matunda huonesha mti ulivyotunzwa,

vivyo hivyo maneno ya mtu humjulisha alivyo.

7Usimsifu mtu ambaye hajaongea

kwa vile mtu hupimwa kwa maneno yake.

Uaminifu

8Ukitaka kuwa mwema utafanikiwa kuwa mwema,

na kuuvaa wema kama vazi la sikukuu.

9Ndege hujumuika na ndege wa aina yao,

ndivyo na ukweli unavyoandamana na wale wanaoutekeleza.

10Kama vile simba anavyootea mawindo,

ndivyo na dhambi inavyowaotea watendao uovu.

11Mazungumzo ya wenye kumcha Mungu ni ya hekima daima,

lakini mpumbavu hubadilika kama mwezi.

12Ukijikuta miongoni mwa wapumbavu ondoka;

lakini miongoni mwa wenye busara, kaa.

13Mazungumzo ya wapumbavu ni kinyaa,

na kucheka kwao ni ufisadi wa dhambi.

14Kuongea kwa watu hao hukufanya ushtuke kabisa,

na mabishano yao humfanya mtu azibe masikio.

15Ugomvi wa wenye majivuno husababisha mauaji,

na matusi yao ni aibu kuyasikiliza.

Kutoa siri

16Anayetoa siri anakosa uaminifu wote,

na kamwe hatapata rafiki anayemtaka.

17Mpende rafiki na uwe na imani naye,

lakini kama umetoa siri zake, usiandamane naye tena.

18Maana, kama mtu anavyomwangamiza adui

wewe nawe umeharibu urafiki wa jirani yako.

19Kama ulivyomwachilia ndege achopoke mkononi mwako,

hivyo umemwachilia jirani yako,

wala hutaweza kumpata tena.

20Usimfuate, maana amekwenda mbali sana,

amekimbia kama paa aliyenusurika kwenye mtego.

21Kidonda chaweza kutibiwa, na kutukanwa kusamehewa;

lakini aliyetoa siri, asitumaini lolote.

Unafiki

22Anayepepesa macho anakusudia kutenda maovu,

wala hakuna mtu anayeweza kumvumilia.

23Mtu huyo awapo nawe, anayosema ni matamu,

na atayafurahia unayomwambia.

Lakini baadaye, atabadilisha usemi wake,

na kukunasa kwa maneno yako mwenyewe.

24Maishani nimeyachukia mambo mengi,

lakini mtu kama huyo namchukia kuliko yote,

hata Bwana anamchukia mtu kama huyo.

25Anayetupa jiwe juu angani analitupa kichwani mwake mwenyewe.

Apigaye ngumi hujiumiza mwenyewe.

26Mchimba shimo hutumbukia yeye mwenyewe,

na mtega mtego hunaswa mwenyewe.

27Mtu akitenda uovu, uovu utampata,

wala hatajua umetoka wapi.

28Mwenye majivuno hudhihaki na kudharau,

lakini adhabu inamngojea kama simba.

29Wanaofurahia kuanguka kwa wenye kumcha Mungu,

watanaswa katika mtego

na maumivu yatawakumba kabla ya kufa kwao.

Chuki

30Hasira na ghadhabu, yote ni machukizo,

na mwenye dhambi atayapata yote hayo.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania