Sira 32

Sira 32

Karamu

1Kama ukifanywa msimamizi wa karamu usivimbe kichwa,

ila ujifanye kama wengine karamuni;

wahudumie vizuri kwanza kisha ukae.

2Ukisha timiza wajibu wako, keti mahali pako,

ujifurahishe pamoja na wengine

na kupewa shada la heshima kwa kazi yako njema.

3Ikiwa wewe ni mzee kwa umri zungumza;

lakini ongea kwa busara, usikatishe muziki.

4Kama kunatolewa vinywaji usirefushe mazungumzo yako.

Usioneshe elimu yako wakati usio wake.

5Muziki kwenye karamu ya pombe

ni kama mhuri wa kito juu ya dhahabu.

6Muziki mtamu pamoja na pombe

ni kama mhuri wa zumaridi juu ya dhahabu.

7Ikiwa wewe ni kijana, ongea kama ni lazima;

lakini si zaidi ya mara mbili na iwe umeombwa.

8Ongea wazi, useme mengi kwa machache;

onesha kuwa wajua mengi ila hupendi kusema.

9Ukiwa miongoni mwa wakuu usijifanye sawa nao,

usiseme maneno ya porojo wakati mwingine anaongea.

10Kama umeme unavyotangulia ngurumo,

ndivyo heshima inavyotangulia mtu anayejiheshimu.

11Ondoka karamuni wakati unaofaa, usiwe wa mwisho;

nenda nyumbani upesi wala usingojengoje.

12Jifurahishe na kufanya unachotaka,

lakini usitende dhambi kwa maneno ya majivuno.

13Kwa ajili ya mambo haya mtukuze Mungu aliyekuumba

na kukuridhisha kwa zawadi zake nzuri.

Uchaji

14Amchaye Bwana, hukubali kukosolewa naye,

na anayemtafuta mapema atapata baraka zake.

15Anayeitafuta sheria, ataridhika kuipata,

lakini mnafiki atapata kikwazo.

16Wamchao Bwana watajua kutenda sawa,

na matendo yao yatangaa kama mwanga.

17Wenye dhambi hawakubali kukosolewa;

hupata kisingizio kufanya watakavyo.

18Mwenye busara hapuuzi maoni ya mtu,

lakini mtu fidhuli na mwenye majivuno haogopi kitu.

19Usifanye chochote bila kufikiri,

nawe hutalazimika kujuta baada ya kufanya kitu.

20Usifuate njia yenye vikwazo vingi,

usije ukajikwaa juu ya mawe.

21Usiwe na imani mno na njia iliyonyoka,

22ila uwe mwangalifu sana juu ya njia yako.

23Uchukue hadhari katika kila kitendo,

maana hii ndiyo maana ya kuzishika amri.

24Anayeiamini sheria atazitii na amri,

na anayemtegemea Bwana hatapata madhara.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania