Sira 41

Sira 41

Kifo

1Ewe kifo! Kukukumbuka ni uchungu mkubwa,

kwa mtu anayeishi kwa amani na mali zake;

kwa mtu asiye na wasiwasi, anayefanikiwa kila kitu,

na aliye bado na nguvu za kufurahia chakula chake.

2Ewe kifo! Hukumu yako ni jambo jema sana

kwa fukara na ambaye nguvu zake zinamwishia,

kwa mtu mzee sana mwenye wasiwasi juu ya kila kitu,

mtu mwenye uchungu na ambaye ameishiwa na uvumilivu.

3Usiogope maamuzi ya kifo;

kumbuka waliokutangulia na watakaokufuata.

4Hiyo ni kauli ya Bwana kwa viumbe vyote.

Kwa nini basi kupinga alichopenda kuamua Mungu Mkuu?

Kuishi miaka kumi au mia au elfu,

hiyo si hoja huko ahera.

5Watoto wa wenye dhambi ni chukizo;

hurandaranda katika makao ya wasiomcha Mungu.

6Urithi wa watoto wa wenye dhambi utapotea,

na wazawa wao wataishi katika aibu daima.

7Watoto watamlaani baba asiyemcha Mungu,

kwa sababu ya aibu aliyowaletea wanawe.

8Ole wenu, nyinyi msiomcha Mungu,

nyinyi ambao mmeiacha sheria ya Mungu Mkuu!

9Mkifanikiwa, mapato yenu yatatoweka;

mkijikwaa, hamtaweza kuinuka tena;

na mtakapokufa, laana ndiyo mtakayopata.

10Chochote kilichotoka mavumbini hurudi mavumbini,

wabaya huanza na laana na kuishia maangamizini.

11Watu huomboleza juu ya miili ya marehemu,

lakini jina baya la wenye dhambi litafutiliwa mbali.

12Ulipe hadhi jina lako kwani litakubakia,

litadumu kuliko hazina elfu moja za dhahabu.

13Wakati wa furaha ni wa muda tu,

lakini jina zuri hudumu milele.

Kuwa na haya

14Wanangu, zingatieni mafundisho yangu mkae na amani.

Hekima iliyofichika na hazina isiyoonekana,

je hivyo vina faida gani?

15Afadhali mtu anayeficha ujinga wake,

kuliko yule anayeficha hekima yake.

16Kwa hiyo uyaheshimu maneno yangu;

maana si vizuri kuona haya juu ya kila kitu

na si kila hali inakubaliwa kuwa sawa na wote.

17Uone haya juu ya kufanya machafu mbele ya wazazi,

juu ya kusema uongo mbele ya mkuu au mtawala,

18juu ya kukosa mbele ya hakimu au mwamuzi,

juu ya kufanya uovu mbele ya jumuiya,

19juu ya kumdanganya mwenzako wa kazi au rafiki,

juu ya wizi mahali unapoishi.

20Uone haya juu ya kukosa uaminifu mbele ya Mungu na agano lake,

juu ya utovu wa adabu wakati wa kula,

21juu ya kuwa mchoyo unapoombwa kitu,

juu ya kukaa kimya unaposalimiwa,

22juu ya kumwangalia mwanamke malaya,

juu ya kukataa kumsaidia mtu wa jamaa,

23juu ya kumnyanganya mtu mali yake,

juu ya kumkodolea macho mke wa mwenzako,

24na juu ya kumshawishi mtumishi wake wa kike;

tena usiende karibu na kitanda chake.

25Uone haya kutumia lugha chafu mbele ya rafiki,

na wala usimkaripie mtu unayempa zawadi.

26Uone haya juu ya kurudia na kusema fununu,

na kutoa siri za watu.

27Hiyo ndiyo kuwa na haya halali,

ambayo kila mtu anapenda.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania