Sira 8

Sira 8

Kutumia akili

1Usishindane na mtu mwenye uwezo,

la sivyo utajikuta makuchani mwake.

2Usigombane na mtu yeyote tajiri,

la sivyo utajiri wake utakushinda mahakamani.

Maana dhahabu imewaangamiza wengi

na kuipotosha mioyo ya wafalme.

3Usibishane na mtu anayepayukapayuka;

usiongeze kuni katika moto wake.

4Usitaniane na mtu asiye na adabu,

la sivyo atawafedhehesha wazee wako.

5Usimdharau mtu aliyetubu dhambi.

Kumbuka sote tuna hatia.

6Usimbeze mtu yeyote aliye mzee,

maana baadhi yetu tunakuwa wazee.

7Usifurahie kifo cha mtu yeyote.

Kumbuka sisi sote lazima tufe.

8Usidharau misemo ya wenye hekima

bali jitahidi kufahamu mafumbo yao;

maana kutokana na hayo utajifunza mbinu

na mtindo wa kuwatumikia wakuu.

9Usipuuze wanayosema wazee,

maana wao pia walifunzwa na baba zao.

Utajifunza kutoka kwao namna ya kufikiri

na ufundi wa kutoa jibu wakati wake.

10Usichochee moto wa mwenye dhambi;

usije ukajichubua nawe kwa moto wake.

11Usikubali kuongozwa na fidhuli,

asije akajaribu kukunasa kwa maneno yako.

12Usimkopeshe mtu mwenye nguvu kuliko wewe;

kama ukimkopesha kitu, ujue kuwa kimepotea.

13Usitoe dhamana kuliko uwezo wako,

ukiwa mdhamini, basi uwe tayari kulipa.

14Usimshtaki hakimu mahakamani,

maana hukumu itatolewa kwa kumpendelea yeye.

15Usisafiri pamoja na mtu mzembe,

asije akawa mzigo kwako;

maana atatenda aongozwavyo na hisi zake,

nanyi wawili mtaangamia kwa ujinga wake.

16Usibishane na mtu akasirikaye haraka,

wala usisafiri naye mahali kusiko na watu;

maana kwake kumwaga damu si kitu,

na huko kusiko na msaada, atakushambulia.

17Usiombe ushauri kwa mtu mpumbavu,

maana yeye hataweza kutunza siri.

18Usifanye lolote la siri mbele ya mgeni,

maana hujui atafanya nini na siri hiyo.

19Usimfungulie kila mtu yaliyo moyoni mwako,

wala usikubali yeyote akupendelee.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania