Wimbo Ulio Bora 1

Wimbo Ulio Bora 1

1Wimbo wa Solomoni ulio bora kuliko nyimbo zote.[#Taz 1 Fal 4:32; #1:1 Au Kwa heshima ya Solomoni, au juu ya Solomoni.]

Shairi la kwanza

Bibi arusi

2Heri midomo yako inibusu,

maana pendo lako ni bora kuliko divai.

3Manukato yako yanukia vizuri,

na jina lako ni kama marashi yaliyomiminwa.

Kwa hiyo wanawake hukupenda!

4Nichukue, twende zetu haraka,

mfalme amenileta katika chumba chake.

Tutafurahi na kushangilia kwa sababu yako,

tutasifu mapenzi yako kuliko divai.

Wanawake wana haki kukupenda!

5Enyi wanawake wa Yerusalemu,

mimi ni mweusi na ninapendeza,

kama mahema ya Kedari,

kama mapazia ya Solomoni.

6Msinishangae kwa sababu ni mweusi,

maana jua limenichoma.

Ndugu zangu walinikasirikia,

wakanifanya mlinzi wa mashamba ya mizabibu.

Lakini sikutunza shamba langu la mizabibu.

7Hebu niambie ee wangu wa moyo,

utawalisha wapi kondoo wako?

Ni wapi watakapopumzikia adhuhuri?

Kwa nini mimi nikutafute

kati ya makundi ya wenzako?

Bwana arusi

8Ewe upendezaye kuliko wanawake wote;

kama hujui, fanya hivi:

Zifuate nyayo za kondoo;

basi, walishe mbuzi wako karibu na hema za wachungaji.

9Wewe ee mpenzi wangu,

nakulinganisha na farasi dume wa magari ya Farao.

10Mashavu yako yavutia kwa vipuli,

na shingo yako kwa mikufu ya johari.

11Lakini tutakufanyizia mikufu ya dhahabu,

iliyopambwa barabara kwa fedha.

Bibi arusi

12Mfalme alipokuwa kwenye kochi lake,

marashi yangu ya nardo yalisambaa kila mahali.

13Mpenzi wangu ni kama mfuko wa manemane kwangu,

kati ya matiti yangu.

14Mpenzi wangu ni kama maua ya hina yachanuayo,

kwenye mashamba ya mizabibu huko Engedi.

Bwana arusi

15Hakika u mzuri, ee mpenzi wangu,

hakika u mzuri!

Macho yako ni kama ya hua!

Bibi arusi

16Hakika u mzuri ewe nikupendaye,

u mzuri kweli!

Majani mabichi yatakuwa kitanda chetu;

17mierezi itakuwa nguzo za nyumba yetu,

na miberoshi itakuwa dari yake.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania