The chat will start when you send the first message.
1Hekima aliwafanikisha hao watu
wakiongozwa na yule nabii mtakatifu.
2Walisafiri jangwani pasipokaliwa na watu,
wakapiga hema zao mahali ambapo hakuna aliyepitia kabla.
3Waliwakabili maadui zao na kuwashinda wapinzani wao.
4Walipoona kiu walikulilia,
nawe ukawapa maji kutoka kwenye mwamba mgumu,
wakakata kiu yao.
5Pigo ulilowapa maadui zao
liliwasalimisha watu wako taabuni.
6Badala ya maji ya mto unaotiririka daima,
mto uliofurika na kutiwa unajisi kwa damu
7kama adhabu kwao walioamuru watoto wachanga wauawe
wewe uliwapatia watu wako maji mengi ghafla,
8ukaonesha kwa kiu yao wakati ule,
jinsi ulivyowaadhibu maadui zao.
9Walipojaribiwa, ingawa walikuwa wanapewa nidhamu kwa huruma,
walijifunza jinsi waovu walivyoteswa wakati ulipowahukumu kwa hasira.
10Uliwaonya kama vile baba aonyavyo watoto wake.
Lakini uliwachunguza hao waovu kama mfalme mkali anapohukumu.
11Wakiwa mbali au wakiwa karibu wote waliteseka,
12Walipata majonzi maradufu
kwa kukumbuka yaliyotukia.
13Waliposikia kwamba adhabu yao iliwafaidia watu wako,
walikiri kwamba wewe, ee Bwana, ndiwe uliyeyatenda hayo.
14Ingawa walikuwa wamemdharau yule ambaye
hapo awali alikuwa ametupwa na kuachwa,
baada ya matukio hayo yote walimstaajabia,
waliposikia kiu kali kuliko ya watu waadilifu.
15Kwa sababu ya upumbavu na mawazo yao maovu
ambayo yaliwapotosha wakaabudu nyoka na wanyama duni,
wewe uliwaleta viumbe wasio na akili wawaadhibu,
16wajifunze kwamba mtu huadhibiwa
kwa vitu vilevile alivyotenda navyo dhambi.
17Kwa mkono wako wenye nguvu zote
ambao uliumba ulimwengu bila kutumia chochote chenye umbo,
umekuwa daima wenye uwezo
na ungaliweza kwa urahisi kuwaletea dubu wengi au simba wakali,
18au wanyama wakali sana ambao hawajapata kuwako,
au wanyama watoao pumzi ya moto
au wanaopumua moshi mzito wenye kudhuru,
au watoao machoni mwao cheche za kutisha.
19Sio tu kwamba mashambulio ya hao wanyama yangeua watu
ila kule tu kuwaona watu wangekufa kwa kutishwa.
20Licha ya hao, ungaliweza kuwaangamiza kwa pumzi moja tu
wakifuatiwa na haki yako,
au kuwatawanya kila mahali kwa mvumo wa uwezo wako.
Lakini wewe umepanga kufanya kila kitu kwa kipimo, taratibu na uzito.
21Kuwa na uwezo mkuu ni hadhi yako daima,
na hakuna mtu awezaye kuikabili nguvu ya mkono wako.
22Kwako, ulimwengu wote ni kama chembe moja katika mizani;
ni kama tone moja la umande wa asubuhi juu ya ardhi.
23Lakini wewe ni mwenye huruma kwa wote maana waweza yote;
waacha kuzijali dhambi zetu ili tupate kutubu.
24Wewe wapenda vitu vyote vilivyopo,
wala huchukii chochote ulichokiumba.
Hungaliumba chochote kile kama ungekuwa unakichukia.
25Chawezaje chochote kudumu ila kwa kupenda kwako?
Chawezaje kuendelea kuwako kama hungalikiumba?
26Umeruhusu vitu vyote viwepo ee Bwana,
kwa maana ni vyako, nawe wapenda vitu vyote hai.