The chat will start when you send the first message.
1Lakini wewe, Mungu wetu, ni mwenye wema na kweli,
wewe ni mvumilivu na watawala vyote kwa huruma.
2Hata tukitenda dhambi twajua nguvu yako, nasi tu watu wako.
Lakini hatutatenda dhambi kwa kuwa tunajua kwamba sisi ni wako.
3Maana kukujua wewe ni uadilifu kamili,
kutambua nguvu yako ni chanzo cha kuishi milele.
4Sisi hatukupotoshwa kwa kazi mbaya za ufundi wa binadamu,
au kwa kitu duni kilichotiwa nakshi na msanii,
kinyago kilichopakwa rangi mbalimbali,
5ambacho umbo lake huamsha tamaa za watu wajinga
na kuwafanya watamani sanamu isiyo na uhai wowote.
6Wanaotengeneza vitu kama hivyo,
na wanaotamani kuviabudu,
wote wangangania uovu.
7Mfinyanzi huukanda udongo laini
akafinyanga kila chombo kwa uangalifu kwa matumizi yetu.
Hutumia udongo huo huo kufinyangia vyombo:
Vingine kwa matumizi safi
na vingine kwa matumizi yasiyo safi.
Vyombo vyote hivyo huviunda namna moja.
Lakini ni vyombo vipi kwa matumizi yapi,
mfinyanzi mwenyewe huamua.
8Tena kwa kazi bure mfinyanzi huunda mungu duni kwa udongo ule ule,
hali yake mwenyewe ni kiumbe kifacho kilichoundwa hivi, punde tu
na wakati ufikapo wa kurudisha roho yake aliyokopeshwa,
atarudi udongoni ambamo alitolewa.
9Lakini yeye hajali kwamba kifo kinamkabili,
wala kwamba maisha yake ni mafupi;
ila hushindana na mafundi wa vyombo vya dhahabu na fedha
na kuiga mafundi watumiao shaba,
na kuona fahari kwa kufinyanga miungu ya kuiga.
10Moyo wake ni majivu na tumaini lake ni hafifu kuliko vumbi.
Uhai wake hauna thamani kama udongo,
11kwa sababu hajapata kamwe kumtambua Mungu aliyemwumba,
Mungu aliyemjalia roho mwenye nguvu ya kutenda,
alimpulizia pumzi ya uhai.
12Mtu huyo hufikiria maisha yetu kuwa mchezo tu,
na uhai wetu kuwa tamasha la kujipatia faida.
Husema ni lazima kupata fedha kwa vyovyote vile
hata kama ni kwa njia isiyofaa.
13Mtu huyo ambaye kwa udongo ule ule hufinyanga sanamu za miungu na vyombo vivunjikavyo,
ajua kuliko wengine wote kwamba anatenda dhambi.
14Lakini wapumbavu kuliko wote na wanaosumbuka kuliko watoto wachanga,
walikuwa wale maadui ambao waliwatesa watu wako.
15Wao walidhani sanamu za watu wasiomjua Mungu ni miungu,
ingawaje hazina macho ya kuona
wala pua za kuvuta pumzi,
wala masikio ya kusikia,
wala vidole vya kupapasa,
na miguu yao haifai kitu kwa kutembea.
16Binadamu ndiye aliyezitengeneza,
mtu ambaye roho yake amekopeshwa ndiye aliyezifanya.
Hakuna mtu awezaye kutengeneza mungu aliye bora kuliko binadamu.
17Mtu hufa, lakini hutengeneza kitu ambacho chenyewe kimekufa fofofo.
Yeye binafsi ni bora kuliko hicho kitu anachokiabudu.
Naam, yeye ana uhai, lakini hicho kitu anachokiabudu hakina uhai kabisa.
18Watu hao huabudu hata wanyama wa kuchukiza kabisa
ambao hata kwa akili ni duni kuliko viumbe vingine vyote.
19Hata ukivilinganisha na viumbe vingine, hivi havitamaniki kabisa.
Vyenyewe havikuwahi kupata sifa na baraka ya Mungu.