Hekima ya Solomoni 3

Hekima ya Solomoni 3

1Lakini watu wanyofu wako mikononi mwa Mungu,

Mateso yoyote hayatawapata kamwe.

2Kwa wapumbavu walionekana kwamba wamekufa

na kwamba kufariki kwao kulikuwa jambo baya;

3kuondoka kwao kwetu kulidhaniwa kuwa uharibifu,

lakini ukweli ni kwamba wamo katika amani.

4Waonavyo watu ni kwamba wameadhibiwa,

lakini wanalo tumaini thabiti la kutokufa.

5Waliadhibiwa kidogo tu,

lakini sasa watapokea tuzo kubwa;

Mungu aliwajaribu akawapata wanastahili kuishi kwake.

6Aliwajaribu kama dhahabu katika tanuri,

akawapokea kama tambiko ya kuteketezwa.

7Wakati wa kupata tuzo utakapofika, watangaa,

watameremeta kama vimulimuli katika nyasi kavu.

8Watayahukumu na kuyatawala makabila na mataifa,

naye Bwana atatawala juu yao milele.

9Wote wamwaminio Mungu watatambua ukweli wake;

wote walio waaminifu watakaa kwake kwa upendo,

maana huwajalia neema na huruma watakatifu wake,

na huwaangalia kwa wema hao aliowateua.

10Lakini wabaya wataadhibiwa kadiri ya fikira zao mbovu,

naam, wasiojali mambo ya uadilifu,

wote waliomwasi Bwana.

11Wote wanaodharau hekima au nidhamu wana bahati mbaya;

tumaini lao ni bure,

jasho lao haliwafaidii chochote;

na matendo yao ni ya bure.

12Wake zao huwa wapumbavu na watoto wao wapotovu;

wazawa wao watakuwa katika laana.

Umuhimu wa fadhila

13Heri mwanamke tasa ambaye hana hatia

ambaye hajahusika na muungano ulio dhambi;

huyo atapata tuzo Mungu atakapohukumu roho za watu.

14Heri pia towashi asiyevunja sheria kwa mikono yake,

ambaye hajafikiria maovu dhidi ya Bwana;

huyo atapata upendeleo maalumu kwa uaminifu wake,

na mahali pa furaha kuu katika hekalu la Bwana.

15Maana matunda ya kazi njema ni utukufu;

ni kama mizizi welekevu inayochipua daima.

16Lakini watoto wa wazinzi watakufa kabla ya kukomaa;

naam, wazawa wa wazinzi wataangamia.

17Na hata wakiishi sana hakuna atakayewajali,

na hatimaye uzee wao hautakuwa na heshima.

18Wakifa vijana hawatakuwa na tumaini,

wala hawatapata kitulizo wakati wa hukumu.

19Maana mwisho wa watu wasio waadilifu ni balaa tupu.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania