The chat will start when you send the first message.
1Katika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku ya kumi na tatu ilikuwa ile siku iliyotangazwa kwamba: Lile neno la mfalme, aliloliagiza, lifanyike siku hiyo; ndipo, adui za Wayuda walipongojea kuwashinda, lakini ikageuzwa, Wayuda wakapata wao kuwashinda wachukivu wao.
2Siku hiyo ilipotimia, Wayuda wakakusanyika katika miji yao katika majimbo yote ya mfalme Ahaswerosi kuwaua kwa mikono yao waliotaka kuwafanyizia mabaya, lakini hakuwako mtu aliyesimama mbele yao, kwani mastusho yaliyaguia makabila yote.[#Est. 8:17.]
3Nao wakuu wote wa majimbo nao wenye amri nao watawala nchi nao wenye kazi nyingine za mfalme wakawasaidia Wayuda, kwani woga uliwaguia wa kumwogopa Mordekai.
4Kwani Mordekai alikuwa mkubwa katika nyumba ya mfalme, nayo sifa yake ikasikilika katika majimbo yote, kwani huyo mtu Mordekai akaendelea kuwa mkubwa zaidi.
5Wayuda wakawapiga adui zao wote mapigo ya panga, wakawaua, wakawaangamiza, wakawafanyizia wachukivu wao, kama walivyopendezwa.
6Namo Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, wakaua watu, wakaangamiza watu 500.
7Wakawaua nao hawa: Parsandata na Dalfoni na Asefata
8na Porata na Adalia na Aridata
9na Parmasta na Arisai na Aridai na Yezata;
10ndio wana kumi wa Hamani, mwana wa Hamedata, aliyekuwa mpingani wao Wayuda; lakini mali zao hawakuziteka kwa mikono yao.
11Siku hiyo mfalme alipopata hesabu yao waliouawa Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme,
12mfalme akamwambia Esteri, mkewe mfalme: Humu susani, mlimo na jumba la mfalme, Wayuda wameua na kuwaangamiza watu 500 na wana kumi wa Hamani; sijui, waliyoyafanya katika majimbo mengine ya mfalme yaliyosalia. Lakini unayoyaomba utapewa; nayo unayoyataka yatafanyika tena.[#Est. 5:6; 7:2.]
13Esteri akasema: Vikiwa vema kwake mfalme, Wayuda waliomo Susani wapewe ruhusa hata kesho kufanya, kama walivyofanya leo, nao wale wana kumi wa Hamani wawatundike katika ule mti.
14Mfalme akasema: Na yafanyike hivyo! Kisha hiyo amri ya mfalme ikatolewa mle Susani, nao wale wana kumi wa Hamani wakawatundika.
15Basi, Wayuda waliokuwamo Susani wakakusanyika hata siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, wakaua mle Susani tena watu 300, lakini mali zao hawakuziteka kwa mikono yao.
16Nao wale Wayuda wengine waliokuwa katika majimbo wakakusanyika, wajisimamie wenyewe na kujiokoa, wajipatie utulivu kwao adui zao, wakaua wachukivu wao 75000, lakini mali zao hawakuziteka kwa mikono yao.
17Hayo yalifanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari, lakini siku ya kumi na nne wakatulia, wakaifanya kuwa siku ya karamu na ya furaha.
18Lakini Wayuda waliokuwa Susani wakakusanyika siku ya kumi na tatu na siku ya kumi na nne, wakatulia siku ya kumi na tano, wakaifanya hiyo kuwa siku ya karamu na ya furaha.
19Kwa sababu hii Wayuda wa mashambani wanaokaa katika miji iliyo wazi huifanya siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kuwa siku ya furaha na ya karamu na sikukuu pia, nao hupeana matunzo mtu na mwenziwe.
20Mordekai akayaandika maneno hayo yote akituma barua kwa Wayuda wote waliokaa katika majimbo yote ya mfalme Ahaswerosi, kwao waliokuwa karibu nako kwao waliokuwa mbali,
21Akawaagiza kuishika desturi hii ya kuzifanya siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari, mwaka kwa mwaka,
22kuwa sikukuu, kwa kuwa ndipo, Wayuda walipopata kutulia kwa adui zao; kwa hiyo ni mwezi, majonzi yao yalipogeuzwa kuwa furaha, nayo masikitiko yao kuwa siku nzuri. Kwa sababu hii wazifanye siku hizo kuwa za karamu na za furaha na za kupeana matunzo mtu na mwenziwe, nao wakiwa sharti wapelekewe vipaji.
23Ndipo, Wayuda walipoitikia kuendelea kuyafanya, waliyoyaanza hapo; ndiyo, Mordekai aliyowaandikia.
24Kwani ndipo, Hamani, mwana wa Hamedata wa Agagi, aliyekuwa mpingani wa Wayuda wote, alipowazia kuwaangamiza Wayuda kwa hivyo, alivyokuwa amewapigia Puri, ndiyo kura, awatoweshe kwa kuwaangamiza.[#Est. 3:7.]
25Lakini mfalme alipopashwa habari hizo alikuwa ameagiza kwa barua kwamba: Wazo hilo baya, alilowawazia kuwafanyizia Wayuda, sharti limrudie kichwani pake, wamtundike yeye na wanawe mtini.[#Est. 7:10; 9:14.]
26Kwa sababu hii sikukuu hizi wakaziita Purimu wakilifuata lile neno la Puri (kura). Kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo na kwa ajili yao, waliyoyaona wenyewe, na kwa ajili yao, wengine waliyowasimulia,
27kwa kuyaitikia yale Wayuda wakaagiza, kwao nako kwao wa uzao wao nako kwao wote watakaojiunga nao iwe desturi isiyotanguka ya kuzishika hizo siku mbili hapo, siku zao zilizowekwa zitakapotimia kila mwaka utakaokuwa, kama yalivyoandikwa.
28Kwa sababu hii sikukuu hizi zikumbukwe, zishikwe kwa kila kizazi na kwa kila mlango katika kila jimbo na katika kila mji; hizo sikukuu za Purimu zisikome kabisa kwao Wayuda, wala ukumbusho wao usitoweke kwao wa uzao wao.
29Kisha Esteri, mkewe mfalme, mwana wa Abihaili, na Myuda Mordekai wakaandika barua ya pili na kuwashurutisha watu kwelikweli na kuwaagiza kuzishika hizo sikukuu za Purimu.
30Akatuma hiyo barua kwa Wayuda wote katika yale majimbo 127 ya ufalme wa Ahaswerosi na kuwaambia maneno ya utengemano wa kweli.
31Akaagiza kuzishika hizo sikukuu za Purimu siku zilezile, walizowaagiza Myuda Mordekai na Esteri, mkewe mfalme, kama walivyojiagizia wenyewe nao wa uzao wao mambo ya mifungo na ya maombolezo yao.
32Amri ya Esteri iliyoyaagiza mambo ya hizo sikukuu za Purimu ikaandikwa katika kitabu.