The chat will start when you send the first message.
1Nisikieni, ninyi visiwa,
nanyi makabila ya watu mlioko mbali, tegeni masikio!
Bwana aliniita hapo nilipozaliwa,
akalikuza jina langu tangu hapo,
nilipotoka tumboni mwa mama.
2Akakitumikisha kinywa changu kama upanga mkali,
akanificha kivulini mwa mkono wake,
akanitumia kuwa mshale umetukao,
akanificha katika podo lake.
3Akaniambia: Ndiwe mtumishi wangu,
wewe Isiraeli ndiwe, ambaye nitajitukuzia.
4Nami nalisema: Nimejichokesha bure,
nikizimaliza nguvu zangu na kusumbukia mambo
yasiyo na maana, yasiyo kitu.
Lakini yanipasayo yako na Bwana,
mapato yangu yako na Mungu wangu.
5Sasa nimeambiwa neno na Bwana
aliyenitengeneza tumboni mwa mama
kuwa mtumishi wake wa kumrudisha Yakobo kwake,
Waisiraeli wapate kukusanyika kwake;
kwani nimetukuka machoni pa Bwana,
Mungu wangu akawa nguvu zangu.
6Amesema hivi: Haitoshi, ukiwa mtumishi wangu
wa kuiinua milango ya Yakobo
na wa kuwarudisha Waisiraeli waliookoka,
nimekuweka tena kuwa mwanga wa wamizimu,
wokovu wangu ufike mapeoni kwa nchi.
7Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyemkomboa Isiraeli,
ndivyo, Mtakatifu wake anavyomwambia yeye,
watu wanayembeza na kumchukia mioyoni mwao,
aliye mtumishi wao wanaoitawala nchi:
Wafalme watayaona, nao wakuu watainuka, wakuangukie,
kwa kuwa Bwana ni mtegemevu,
kwa kuwa ndiye Mtakatifu wa Isiraeli aliyekuchagua.
8Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:
Nimekuitikia, siku zilipokuwa za kupendezwa,
nikakusaidia siku ya wokovu,
nikulinde, nikuweke kuwa agano lao walio ukoo wangu,
uichipuze nchi, uwagawie wenyewe mafungu yao yaliyokufa,
9uwaambie wafungwa: Tokeni! nao waliomo gizani: Kesheni!
Watalisha njiani, napo vilimani po pote
palipokuwa pakavu wataona malisho yao.
10Hawataona tena njaa wala kiu,
hawatapigwa na upepo wenye joto wala na jua,
kwani awahurumiaye atawaongoza,
awapeleke kwenye visima vya maji.
11Nayo milima yangu yote nitaiweka kuwa njia,
nazo barabara zangu zitapitia juu.
12Na mwaone watakaotoka mbali:
wengine watatoka upande wa kaskazini,
wengine upande wa baharini, wengine nchi ya Sinimu.
13Shangilieni mbingu! Nawe nchi, piga vigelegele!
Nayo milima na ipige shangwe!
Kwani Bwana amewatuliza walio ukoo wake,
akawahurumia wanyonge walio wake.
14Sioni ulisema: Bwana ameniacha;
Bwana wangu amenisahau.
15Je? Mwanamke humsahau mtoto wake mnyonyaji,
asimhurumie mwana, aliyemzaa?
Ijapo amsahau, mimi sitakusahau kamwe.
16Tazama! Nimekuchora maganjani mwangu,
kuta zako haziondoki machoni pangu.
17Wanao wa kiume wanakuja na kupiga mbio,
lakini wao waliokuvunja na kukubomoa watakutoka.
18Yainue macho yako na kuyazungusha, uone!
Hawa wote wamekusanyika, wafike kwako!
Ndivyo, asemavyo Bwana: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima,
hawa wote utawavaa kama mapambo,
utawatumia kuwa kama ukanda wa mchumba mke.
19Kwani mahame na mapori yako na mashamba yako yaliyokufa
sasa hayatawaeneza watakaokuja, wakae,
nao waliokumeza watakuwa wamekwenda mbali.
20Itakuwa, wanao waliozaliwa katika ukiwa wako
wasemeane masikioni mwako:
Pangu ni padogo, sogeza, ndugu yangu, nipate kukaa!
21Nawe utasema moyoni mwako: Ni nani aliyenizalia hawa?
Mimi nilikuwa sina watoto, maana nilikuwa mgumba,
nilikuwa nimetekwa, nikapelekwa mbali.
Basi, ni nani aliyewakuza hawa,
nilipokuwa nimesazwa peke yangu? Wanatoka wapi hawa?
22Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema:
Tazama! Nitawapungia wamizimu kwa mkono wangu,
nitawatwekea makabila ya watu bendera yangu;
ndipo, watakapowaleta wanao na kuwabeba vifuani,
nao watoto wako wa kike watawachukua mabegani.
23Wafalme watakuwa walezi wako,
nao wake wa kifalme watakuwa wanyonyeshaji wako,
watakuangukia kifudifudi, walambe mavumbi miguuni pako;
ndipo, utakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana,
ya kuwa hawapatwi na soni waningojeao.
24Je? Mwenye nguvu atachukuliwa mateka yake?
Au kole zake mwongofu zitakombolewa?
25Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema:
Kweli nazo kole za mwenye nguvu zitachukuliwa,
nayo mateka ya mkorofi yatapona;
maana wao waliokugombeza nitawagombeza mimi,
nao wanao nitawaokoa mimi.
26Waliokutesa nitawalisha nyama zao,
wanywe damu zao kama ni pombe, mpaka walewe;
ndipo, wote wenye miili ya kimtu watakapojua,
ya kuwa mimi ndimi Bwana, mwokozi wako,
ni mkombozi wako akutawalaye, Yakobo.