Yeremia 22

Yeremia 22

Kuwaonya wafalme wa Yuda.

1Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Shuka kwenda nyumbani mwa mfalme wa Yuda, uliseme mle neno hili,

2kwamba: Sikia, mfalme wa Yuda, ukikaliaye kiti cha kifalme cha Dawidi, wewe na watumishi wako nao walio wa ukoo wako mnaoingia humu malangoni!

3Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Fanyeni yaliyo sawa yaongokayo! Waponyeni walionyang'anywa na kuwatoa mikononi mwa wakorofi! Wageni nao waliofiwa na wazazi na wajane msiwaonee, wala msiwakorofishe! Wala damu zao wasiokosa msizimwage mahali hapa![#Yer. 21:12.]

4Kwani kama mtalifanya kweli neno hili, wataingia malangoni mwa nyumba hii wafalme wanaokikalia kiti cha kifalme cha Dawidi, wanaopanda magari na farasi, wao wenyewe na watumishi wao na watu wao.[#Yer. 17:25.]

5Lakini msipoyasikia maneno haya, basi, nimejiapia mwenyewe, nyumba hii itakuwa mavunjiko; ndivyo, asemavyo Bwana.

6Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyoisemea nyumba ya mfalme wa Yuda: Kwangu wewe u kama Gileadi ulio mlima mkubwa wa Libanoni; kweli nitakugeuza kuwa nyika yenye miji isiyokaa watu.

7Nitajichagulia waangamizaji wako, kila mtu na mata yake, waikate miangati yako iliyochaguliwa, waitupe motoni!

8Wamizimu wengi watakapopapitia penye mji huu wataulizana mtu na mwenziwe: Kwa sababu gani Bwana ameufanyizia mji huu mkubwa mambo kama hayo?

9Nao watu watawajibu: Ni kwa sababu wameliacha Agano la Bwana Mungu wao, wakaangukia miungu mingine na kuitumikia.

10Msimlilie mfu, wala msimwombolezee! Ila mmlilie sana yeye aliyekwenda! Kwani hatarudi tena, wala hataiona tena nchi, alikozaliwa.

11Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya Salumu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, aliyempokea baba yake ufalme, akatoka mahali hapa: Hatarudi huku tena![#2 Mambo 36:3-4.]

12Kwani mahali, walipomhamishia, ndipo, atakapofia, asiione tena nchi hii.

13Yatampata aijengaye nyumba yake kwa njia isiyoongoka, navyo vyumba vyake vilivyomo kwa njia isiyo sawa; huzitumia kazi za mwenziwe bure tu asipompa mshahara wake.[#Mika 3:10; 3 Mose 19:13.]

14Anasema: Nitajijengea nyumba kubwa yenye vyumba vipana, nitavitobolea madirisha, nitavipigilia juu mbao za miangati, kisha nitavipaka rangi nyekundu.

15Je? Ufalme wako ni kushindana na miangati? Je? Baba yako hakula, hakunywa? Lakini amefanya yaliyo sawa yaongokayo; ndipo, alipopata kukaa vema.

16Akatengenezea wanyonge na wakiwa mashauri yao; ndipo, alipopata kukaa vema; huko siko kunijua? ndivyo, asemavyo Bwana.

17Kwani hakuna mengine, macho yako na moyo wako yanayoyatazamia, ni njia tu za kupata, nazo za kumwaga damu zao wasiokosa, nazo za kukorofisha, nazo za kupenyezewa, uyafanye mambo hayo.

18Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: Hawatamwombolezea kwamba: A ndugu yetu! A umbu letu! Wala hawatamwombolezea kwamba: A bwana! A mwenye utukufu![#Yer. 34:5.]

19Atazikwa, kama punda anavyozikwa, akikokotwa na kutupwa nje kwenye malango ya Yerusalemu.[#Yes. 14:19.]

20Panda Libanoni, ulie! Nako Basani zipaze sauti zako! Nako toka Abarimu vilio vyako visikilike! Kwani wote waliokupenda wamepondwa.

21Nilikuambia neno, ulipokuwa umetulia vema, ukajibu: Sisikii! Hii ndiyo njia yako tangu ujana wako, kwani hukuisikia sauti yangu.

22Upepo utawachunga wachungaji wako wote, nao waliokupenda watakwenda kufungwa; ndipo, utakapoona soni na kuiva uso kwa ajili ya ubaya wako wote.[#Yer. 25:9,18.]

23Unakaa kama ndege ya Libanoni katika tundu kwenye miangati; lakini utapaswa na kuhurumiwa, machungu yatakapokujia yatakayokuwa kama uchungu wa mzazi.[#Yer. 13:21.]

24Ndivyo, asemavyo Bwana: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, kama wewe Konia, mwana wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yenye muhuri mkononi pangu pa kuume, ningekuondoa kwa nguvu,[#Yer. 24:1.]

25nikakutia mikononi mwao waitafutao roho yako namo mikononi mwao, unaowaogopa sana, namo mikononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, namo mikononi mwa Wakasidi.

26Tena wewe na mama yako aliyekuzaa nitawabwaga katika nchi nyingine isiyo yenu ya kuzaliwa; ndiko, mtakakofia.[#2 Fal. 24:12,15.]

27Lakini katika nchi hii, wanayoitunukia rohoni mwao, hawatarudi huku.

28Je? Huyu mtu Konia siye chungu kinachowaziwa si kitu, kinachovunjwa tu? Siye chombo kisichopendwa? Mbona yeye nao walio kizazi chake wamebwagwa na kutupwa katika nchi, wasiyoijua?

29E nchi, nchi, nchi, lisikie Neno lake Bwana!

30Ndivyo, Bwana anavyosema: Mwandikeni mtu huyu kuwa pasipo watoto, kuwa mtu asiyejipatia mema siku zake zote, hata katika kizazi chake hamna mtu atakayejipatia kukikalia kiti cha kifalme cha Dawidi na kuwatawala Wayuda tena.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania