Yosua 6

Yosua 6

Mji wa Yeriko unatekwa.

1Wayeriko walikuwa wamefunga malango, nayo yakakaa hivyo, yalivyofungwa wa ajili ya wana wa Isiraeli, hakuwako aliyetoka wala aliyeingia.

2Bwana akamwambia Yosua: Tazama, huu mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake na mafundi wa vita walio wenye nguvu nimeutia mkononi mwako.

3Uzungukeni mji huu, ninyi wapiga vita wote, mwuzunguke wote pia mara moja! Fanyeni hivyo siku sita!

4Tena watambikaji saba na washike mabaragumu saba yenye milio mikubwa, walitangulie Sanduku la Agano! Siku ya saba sharti mwuzunguke mji huu mara saba, watambikaji wakiyapiga mabaragumu yao.[#3 Mose 25:9.]

5Tena pembe ya kondo yenye mlio mrefu itakapopigwa, watu watakapozisikia sauti za mabaragumu, watu wote pia na wazomee mazomeo makubwa, ndipo, kuta za boma la mji zitakapoanguka chini, watu wenu wapate kupanda na kuingia mjini kila mtu hapo, anaposimama.

6Ndipo, Yosua, mwana wa Nuni, alipowaita watambikaji, akawaambia: Lichukueni Sanduku la Agano! Tena watambikaji saba na wachukue mabaragumu saba yenye milio mikubwa, walitangulie Sanduku la Bwana.

7Nao watu akawaambia: Nendeni kuuzunguka mji huu wote! Nao wenye mata na walitangulie Sanduku la Bwana!

8Yosua alipowaagiza watu hivyo, watambikaji saba wakachukua mabaragumu saba yenye milio mikubwa kwenda mbele ya Bwana, nao wakaenda wakiyapiga hayo mabaragumu, nalo Sanduku la Agano la Bwana likawafuata.

9Nao wenye mata walikwenda mbele ya watambikaji waliopiga mabaragumu, nao wafuasi wa nyuma walikwenda nyuma ya Sanduku hilo, wote walikuwa wanakwenda, mabaragumu yakilia.

10Lakini wale watu Yosua alikuwa amewaagiza kwamba: Msizomee! Wala sauti zenu zisisikilike! Wala neno lo lote lisitoke vinywani mwenu mpaka ile siku, nitakayowaambia: Zomeeni! Hapo ndipo, mtakapozomea.

11Basi, wakalizungusha Sanduku la Bwana na kuuzunguka mji huo wote mzima mara moja, kisha wakaingia makambini, wakalala humo makambini.

12Kesho yake Yosua akaamka na mapema, nao watambikaji wakalichukua Sanduki la Bwana.

13Nao wale watambikaji saba wakayachukua yale mabaragumu yenye milio mikubwa kwenda mbele ya Bwana; basi, walikuwa wanakwenda na kuyapiga hayo mabaragumu, nao wenye mata walikwenda mbele yao, nao wafuasi wa nyuma walikwenda nyuma ya Sanduku la Bwana; wote walikuwa wanakwenda, mabaragumu yakilia.

14Walipokwisha kuuzuguka huo mji mara moja siku ya pili, wakarudi makambini. Nidvyo, walivyofanya siku sita.

15Siku ya saba wakaamka asubuhi, mapambazuko yalipoanza, wakauzunguka huo mji mara saba vivyo hivyo, kama walivyofanya siku zote; lakini siku hiyo wakauzunguka huo mji mara saba.

16Ilipofika mara ya saba, watambikaji wale walipoyapiga mabaragumu, ndipo, Yosua alipowaambia watu: Zomeeni! Kwani Bwana amewapa mji huu.

17Lakini mji uwe wenye mwiko wa kuwapo, yote yaliyomo yawe mali za Bwana. Rahabu tu, yule mwanamke mgoni na apone pamoja nao wote waliomo nyumbani mwake, kwa kuwa aliwaficha wajumbe, niliowatuma.[#4 Mose 21:2; Yos. 2:12-13; Ebr. 11:31.]

18Jiangalieni sana kwa ajili yao yaliyo yenye mwiko, msiyatie kwanza mwiko, kisha mkachukua mengine yaliyo yenye mwiko. Kwani hivyo mtayapatia makambi ya Waisiraeli viapizo kwa kuyaponza[#3 Mose 27:28; 5 Mose 13:17.]

19Fedha zote na dhahabu na vyombo vya shaba na vya chuma ni mali za Bwana, sharti viingie katika kilimbiko cha Bwana.

20Ndipo, watu walipozomea, nayo mabaragumu yakapigwa; watu walipozisikia sauti za mabaragumu, nao wakazidi kuzomea mazomeo makubwa, ndipo, kuta za boma zilipoanguka chini, watu wakapanda kuuingia mji kila mtu hapo, aliposimama; ndivyo, walivyouteka huo mji.[#Ebr. 11:30.]

21Wote waliokuwamo mjini wakawatia mwiko wa kuwapo, wakawaua kwa ukali wa panga, waume kwa wake, watoto kwa wazee, hata ng'ombe na kondoo na punda.

Rahabu nao wa mlango wake wanapona.

22Wale watu wawili walioipeleleza nchi hiyo Yosua akawaambia: Ingieni nyumbani mwake yule mwanamke mgoni, mmtoe mle nyumbani yule mwanamke nao wote waliomo mwake, kama mlivyomwapia.[#Yos. 2:14.]

23Ndipo, wale wapelelezi vijana walipoingia mwake, wakamtoa Rahabu na baba yake na mama yake na ndugu zake nao wote waliokuwa kwake, nao wote wa ukoo wake wakawatoa, wakawaweka mahali palipokuwa nje ya makambi ya Waisiraeli.[#4 Mose 31:19.]

24Kisha huo mji wakauteketeza kwa moto pamoja navyo vyote vilivyokuwamo, lakini fedha na dhahabu na vyombo vya shaba na vya chuma wakavitia katika kilimbiko cha Nyumbani mwa Bwana.

25Lakini yule mwanamke mgoni Rahabu na mlango wa baba yake nao wote waliokuwa wake Yosua akawaacha, asiwaue, naye akakaa katikati ya Waisiraeli mpaka siku hii ya leo, kwa kuwa aliwaficha wajumbe, Yosua aliowatuma kupeleleza Yeriko.[#Amu. 1:25; Mat. 1:5.]

26Kisha Yosua akawaapisha watu hao kwamba: Mtu na awe ameapizwa machoni pa Bwana atakayeinuka, aujenge tena mji huu wa Yeriko! Atakapoweka misingi yake, mwanawe we kwanza atakufa, tena atakapoyatia malango yake, mwanawe mdogo atakufa![#1 Fal. 16:34.]

27Bwana akawa naye Yosua, nao uvumi wake ukasikilika katika nchi yote nzima.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania