The chat will start when you send the first message.
1Kukawa na kilio kikubwa cha watu na cha wake zao kwa ajili ya ndugu zao Wayuda.
2Wakawako waliosema: Sisi wana wetu wa kiume na wa kike ni wengi, sharti tupate ngano, tule, tusife.
3Walikuwako nao wengine waliosema: Mashamba yetu na mizabibu yetu na nyumba zetu hatuna budi kuzitoa kuwa rehani, tupate ngano katika njaa hii.
4Tena walikuwako wengine waliosema: Tumeyatoa mashamba yetu na mizabibu yetu tulipokopa fedha za kulipa kodi ya mfalme.
5Sasa miili yetu si sawa na miili yao ndugu zetu? Nao wana wetu si sawa na wana wao? Tena inakuwaje, tusipokuwa na budi sisi kuwashurutisha wana wetu wa kiume na wa kike kuwa watumwa? Kweli wako wana wetu wa kike waliouzwa utumwani, namo mikononi mwetu hamna cho chote, kwani mashamba yetu na mizabibu yetu ni ya wengine.
6Makali yangu yakawaka moto, nilipokisikia hicho kilio chao na maneno hayo.
7Nikapiga shauri moyoni, nikawagombeza wakuu wa miji na watawalaji nikiwaambia: Ninyi mnawachuuzia vibaya, kila mtu na ndugu yake. Nikawakusanya kuwa mkutano mkubwa na kuteteana nao,[#2 Mose 22:25.]
8nikawaambia: Sisi tuliwakomboa ndugu zetu wa Kiyuda wlaiouzwa kwa wamizimu, kama tulivyoweza; nanyi mtawauza ndugu zenu, waje kujiuza kwetu sisi! Wakanyamaza kimya, hawakuona la kujibu.
9Nikasema: Halifai jambo hili, mnalolifanya ninyi; je? Haiwapasi kufanya mwenendo wa kumwogopa Mungu wetu, adui zetu wa kimizimu wasitutukane?
10Mimi nami na ndugu zangu na vijana wangu tunawakopesha fedha na ngano; lakini sasa deni hizi na tuwaachilie!
11Warudishieni siku hii ya leo mashamba yao na mizabibu yao na michekele yao na nyumba zao nazo faida, mlizowatoza za fedha na za ngano na za mvinyo mbichi na za mafuta!
12Wakaitikia kwamba: Tutavirudisha, tusitake kwao cho chote. Tufanye hivyo, kama unavyosema wewe! Nikawaita watambikaji, nikawaapisha, ya kwamba wafanye, kama walivyosema.
13Kisha nikaikung'uta mikunjo ya nguo zangu nikisema: Hivi ndivyo, Mungu atakavyomkung'uta kila mtu asiyelitimiza neno hili, atoke nyumbani mwake, nayo mapato yake yamtoke; kweli ndivyo, atakavyokung'utwa, awe pasipo kitu kabisa. Mkutano wote ukaitikia: Amin, kisha wakamsifu Bwana, watu wakafanya, kama walivyosema.
14Tangu siku ile, mfalme aliponiweka kuwa mtawala nchi kwao katika nchi ya Yuda, ni tangu mwaka wa ishirini hata mwaka wa thelathini na mbili wa mfalme Artasasta, hii miaka kumi na miwili, wala mimi wala ndugu zangu hatukula chakula cha mtawala nchi.
15Lakini wenye amri walionitangulia waliwalemeza watu wakichukua kwao kila siku chakula na mvinyo za fedha arobaini na zaidi; vijana wao nao waliwakorofisha watu. Lakini mimi sikufanya kama hayo kwa kumwogopa Mungu.
16Hata katika hili jengo la boma nilifanya kazi, lakini hatukununua shamba la watu, nao vijana wangu walikuwa wamekusanywa hapo penye jengo hilo.
17Tena mezani pangu wakala Wayuda na wakuu, watu 150, nao waliokuja kwetu wakitoka kwa wamizimu wanaokaa na kutuzunguka.
18Navyo vyakula vilivyoandaliwa vya kila siku moja, vilikuwa ng'ombe mmoja na kondoo sita waliochaguliwa vema na kuku pia, tena kila siku kumi mvinyo nyingi za kila namna. Kwa hayo yote sikutaka chakula cha mtawala nchi, kwani utumishi uliwalemea watu hawa.
19Mungu wangu, unikumbukie hayo, unirudishie mema kwa ajili ya hayo yote, niliyowafanyizia watu hawa![#Neh. 13:14,22,31.]