Mifano 18

Mifano 18

Urafiki na upatanishi.

1Ajitengaye na watu hutaka kuyafanya, ayatamaniyo

hukataa kwa ukali yote yafaayo.

2Mpumbavu hapendezwi na utambuzi,

hutaka tu kuyafanya yaliyomo moyoni mwake.

3Asiyemcha Mungu anapofika, nayo mabezo hupafika,

tena nayo matusi huja pamoja na matwezo.

4Maneno ya kinywa cha mtu aliye mtu kweli ni maji yenye vilindi,

ni kijito kitoacho maji mengi, ni kisima cha werevu wa kweli.

5Haifai huutazama uso wa mtu aliyekosa

na kumpotoa shaurini asiyekosa.

6Midomo ya mpumbavu huleta ugomvi,

nacho kinywa chake huita mapigo.

7Kinywa cha mpumbavu humwangamiza,

nayo midomo yake ni tanzi liinasalo roho yake.

8Maneno ya msingiziaji ni matamu kama vyakula vya urembo

navyo hushuka tumboni ndani.

9Ailegezaye mikono katika kazi

ni ndugu yake azitawanyaye mali zake.

10Jina la Bwana ni mnara wenye nguvu;

ndipo, mwongofu anapokimbilia, akapona.

11Mali za mkwasi ni ngome yake yenye nguvu,

katika mawazo yake ni boma liendalo juu sana.

12Moyo wa mtu ukijivuna, nyuma huvunjwa,

nayo macheo hutanguliwa na unyenyekevu.

13Kama mtu anajibu akiwa hajasikia bado,

ni ujinga, nao humpatia soni.

14Roho ya kiume huyavumilia magonjwa yake,

lakini roho ikipondeka, yuko nani awezaye kuyavumilia?

15Moyo wa mtambuzi hujipatia ujuzi,

nayo masikio ya walio werevu wa kweli hutafuta ujuzi.

16Vipaji vya mtu humpanulia njia,

tena humfikisha kwa wakuu.

17Atokeaye wa kwanza hushinda shaurini,

mwenziwe anapotokea humwumbua.

18Kura hukomesha magomvi,

huwatenganisha nao wenye nguvu.

19Ndugu apotolewaye hushupaa kuliko mji ulio na boma lenye nguvu,

nayo magomvi yaliyo hivyo hufanana na makomeo ya jumba kubwa.

20Kila mtu hulishibisha tumbo lake mazao ya kinywa chake,

kweli hushiba mazao ya midomo yake.

21Kufa na uzima hushikwa na ulimi,

autunzaye na kuupenda hula mazao yake.

22Aliyepata mkewe amepata kipaji chema,

akijipatia kwa Bwana yampendezayo.

23Maskini husema na kulalamika,

lakini mwenye mali humjibu na kumtolea nguvu.

24Mwenye rafiki wengi huangamia mara nyingi,

lakini yuko rafiki anayeambatana na mtu kuliko ndugu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania