2 Wamakabayo 13

2 Wamakabayo 13

Menelao auawa

1Katika mwaka wa mia moja arubaini na tisa, Yuda na watu wake walisikia ya kuwa Antioko Eupatori alikuwa akiingia Uyahudi na jeshi kubwa.

2Lisia, mtunzaji wake na waziri, alikuwa pamoja naye, na kila mmoja alikuwa na jeshi la Kigiriki la askari elfu mia moja na kumi, wapanda faraasi elfu tano na mia tatu, tembo ishirini na wawili, na magari mia tatu yenye mapanga.

3Menelao pia alijiunga nao, akajipendekeza kwao kwa maneno mengi, si kwa sababu aliifikiri hali njema ya nchi, ila kwa kuwa alitumaini kupata kazi serikali.

4Lakini Mfalme wa wafalme alimtia Antioko hasira juu ya mtu huyu mbaya, hata Lisia alipomwarifu ya kuwa huyu ndiye asili ya matata yote, mfalme aliagiza aletwe Beroya na kuuawa kwa kawaida ya mahali pale.

5Maana huko kuna mnara wenye urefu wa mikono hamsini ambao umejazwa majivu, na ukingo kimeuzunguka pande zote ambacho chateremkia moja kwa moja kwenye majivu.

6Huko huletwa mtu aliyeteka mahekalu au kufanya kosa jingine lililo baya sana, na wote humsukumia mbele kwenye kufa kwake.

7Hiyo ndiyo mauti iliyompata Menelao, mvunja sheria, asipate hata ardhi kwa maziko yake.

8Nayo ilikuwa haki yake, maana alikuwa ametenda dhambi nyingi juu ya madhabahu, ambayo moto wake na majivu yake ni matakatifu; hivyo kwa majivu alikufa.

Vita karibu na mji wa Modini

9Mfalme alikuwa akija kwa hasira kali akikusudia kuwatesa Wayahudi kwa yale mateso makali zaidi yaliyowapata zamani za baba yake.

10Lakini Yuda alipopata habari aliwaagiza watu wamsihi Mungu mchana na usiku, ili,

11kama alivyowaokoa wakati mwingine na awaokoe sasa, maana wamo katika hatari ya kunyang'anywa sheria, na nchi yao, na hekalu takatifu; wala asiwaache hawa waliopata nafuu hivi karibuni tu waanguke katika mikono ya watu wasiomcha Mungu.

12Basi, kwa moyo mmoja walimwomba BWANA siku tatu bila kukoma, wakianguka kifudifudi na kuomboleza na kulia na kufunga. Ndipo Yuda aliwatia moyo akawaambia wajiweke tayari.

13Baada ya kusema faraghani na wazee, alikata shauri watoke na kupigana wawezavyo kwa msaada wa Mungu kabla mfalme hajawahi kuingiza jeshi lake katika Uyahudi na kuutwaa mji.

14Matokeo ya shauri hilo alimwachia Muumba ulimwengu, akawaonya watu wake wapigane kwa ushujaa hata kufa, kwa ajili ya sheria na hekalu na mji na nchi na kawaida zao. Akapiga kambi yake karibu na Modini,

15na baada ya kuwapa askari wake neno la shime, “Kushinda ni kwa Mungu”, yeye na kundi la vijana wateule, hodari sana, walilishambulia hema la mfalme usiku, wakaua watu wa kambini hata elfu mbili, wakawapiga mkuki tembo mkuu na mpandaji wake.

16Mwishowe, wakiisha jaza kambi woga na fujo, waliondoka salama wakati wa mapambazuko.

17Hayo yote yalifanyika kwa msaada wa ulinzi wa Mungu.

Antioko afanya mapatano pamoja na Wayahudi

18Baada ya kuuonja ujasiri wa Wayahudi hivi, mfalme alitumia werevu katika kushambulia maboma yao.

19Akaiendea Bethsura, ngome imara ya Wayahudi, akarudishwa nyuma, akaishambulia tena, akashindwa.

20Naye Yuda aliwapelekea wale wa ndani mahitaji yao ya lazima.

21Ila Rodoko, askari wa Kiyahudi, aliwafunulia adui mambo ya siri; akatafutwa akakamatwa na kufungwa.

22Mfalme akasemezana na watu wa Bethsura tena, akapeana nao yamini, akaondoka. Akalishambulia jeshi la Yuda, akashindwa.

23Akasikia ya kuwa Filipo, aliyeachwa juu ya mambo ya Antiokia, ameasi; habari hiyo ilimtatanisha, akafanya mapatano na Wayahudi, akiyakubali kwa uapo masharti yao ya haki; akiyathibitisha mapatano na kutoa dhabihu. Alilistahi hekalu na mahali patakatifu, na kuonesha mwenendo mwema.

24Kisha alimuaga Yuda kwa makini akaenda Tolemaisi, akimwacha Hegemonide juu ya nchi yote toka Tolemaisi hata Gerari.

25Watu wa Tolemaisi walichukizwa na mapatano hayo wakawakasirikia Wayahudi na kutaka kuyatangua masharti ya maagano.

26Lisia akafika barazani akayatetea awezavyo, akawashawishi na kuwatuliza na kuwaridhisha. Kisha alikwenda Antiokia. Hivyo ndivyo mfalme alivyokuja na kuondoka.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya