The chat will start when you send the first message.
1Yaonekana pia katika maandiko ya kuwa Nabii Yeremia aliwaagiza watakaohamishwa wachukue baadhi ya moto, kama ilivyoandikwa;
2na tena, akiisha kuwapa sheria, aliwaonya wasizisahau amri za Mungu, wala mioyo yao isipotoshwe watakapoona sanamu za dhahabu na fedha na mapambo yake.
3Na kwa maneno mengine ya namna hiyo, aliwasihi wasiache sheria itoke mioyoni mwao.
4Tena, iliandikwa katika maandiko hayo ya kuwa nabii, akionywa na Mungu aliliamuru hema la kukutania na sanduku la Agano yafuatane naye, akiuendea mlima ule Musa alioupanda ili kuutazama urithi wa Mungu.
5Ikawa, alipofikia, aliona pango, mfano wa chumba, na humo alivitia hema na sanduku na madhabahu ya kufukizia uvumba, akauziba mlango wake.
6Wanafunzi wake wengine walikwenda kuiangalia njia, lakini hawakuweza kuiona.
7Aliposikia habari hiyo, Yeremia aliwakemea, akisema, Mahali hapa hapatajulikana hata Mungu awakusanye watu wake tena na kudhihirisha rehema yake.
8Ndipo BWANA atayafunua mambo hayo, na utukufu wa BWANA utaonekana, na lile wingu, kama ulivyoonekana katika siku za Musa, na Sulemani alipoomba mahali patakaswe kwa utukufu.[#Kut 16:10; 24:16; 1 Fal 8:10-11]
9Imeandikwa pia jinsi yeye, kwa hekima yake, alitoa dhabihu wakati wa kulitabaruku hekalu na kulimaliza.
10Kama Musa alivyomwomba BWANA, na moto ukatoka mbinguni ukaiteketeza dhabihu, vivyo hivyo Sulemani aliomba, na moto ukashuka ukaiteketeza sadaka nzima.
11(Musa alisema, kwa kuwa sadaka ya dhambi haikuliwa, ndiyo sababu iliteketezwa).
12Vivyo hivyo Sulemani aliziadhimisha siku nane.
13Mambo hayo yameandikwa pia katika taarifa na maandiko ya Nehemia. Twasoma pia jinsi alivyoanzisha maktaba akakusanya vitabu vyenye habari za wafalme na manabii, na Maandiko ya Daudi, na nyaraka za wafalme juu ya vipaji vitakatifu.
14Yuda naye alitukusanyia hayo maandiko yote yaliyotapanywa kwa sababu ya vita. Tunayo hata sasa;
15basi, kama mkiwa na haja nayo, mwaweza kutuma watu kuyachukua.
16Tu tayari sasa kuiadhimisha sikukuu ya utakaso, ndiyo sababu tunawaandikieni hivi. Nanyi pia mtafanya vema kuziadhimisha siku kuu hizi.[#1 Mak 4:59]
17Mungu aliyewaokoa watu wake wote, na kuwarudishia urithi wao, na ufalme na ukuhani na utakaso,
18kama alivyoahidi katika sheria – katika Mungu tumeweka tumaini letu, kwamba ataturehemu upesi na kutukusanya katika mahali patakatifu kutoka kila mahali chini ya mbingu. Maana ndiye aliyetuokoa katika hatari kubwa, na kupatakasa mahali.
19Habari za Yuda Makabayo na ndugu zake, utakaso wa hekalu kuu, kuitabaruku madhabahu,
20vita juu ya Antioko Epifani na mwanawe Eupatori,
21maono ya mbinguni waliyofunuliwa wale walioishindania dini ya Kiyahudi kwa ushujaa, na jinsi waliovyoiteka nchi yote – ingawa walikuwa watu wachache tu – wakiyakimbiza majeshi ya mataifa,
22na kujitwalia tena hekalu lililosifiwa duniani kote, na kuuweka mji huru, na kukaza tena amri zilizokuwa katika hatari ya kufutika, kwa kuwa BWANA kwa rehema zake aliwafadhili.
23Hayo yote ambayo yamesimuliwa na Yasoni wa Kirene katika vitabu vitano, tutajaribu kuyafupisha kufanya kitabu kimoja tu.
24Wingi wa hesabu zilizomo watatanisha, na masimulizi yake mengi mno yachosha, maana yametiwa hasa kwa ajili yao watakao kuchungua habari za historia.
25Basi, sisi tumewafikiria zaidi wale wanaotaka kujiburudisha kwa masomo na wale wanaotaka kujifunza mambo yaliyotokea, ili tuwafalie wasomaji wetu wote.
26Sisi tuliojitwalia kazi hiyo ngumu ya kufupisha hatukuiona kuwa jambo rahisi, bali ilitaka jasho na kukesha usiku
27kama vile si jambo rahisi kwa mtu kuandalia karamu na kuangalia watu. Lakini haidhuru, tumeishika taabu hiyo kwa furaha ili tustahili shukrani ya watu wengi.
28Tutamwachia mtaalamu wa historia kazi ya kuchunguza kwa uangalifu mambo madogo madogo, na sisi tutajitahidi kwa uaminifu kulifuatisha azimio letu la ufupisho.
29Yampasa fundi mkuu anayeuandalia ujenzi wa nyumba mpya kulifikiria jengo lote; na mwashi atakayelipamba kwa matofali ya rangi na nakshi kuyafikiria yanayofaa kwa mapambo ya kupendeza tu. Nami nailinganisha kazi yetu na ile ya mwashi.
30Ni wajibu wa mwandishi wa historia kuchimbua habari, na kuyahoji mambo yote yanayoihusu, na kuyapeleleza moja moja.
31Lakini yeye anayetengeneza tu mambo yaliyokwisha andikwa ana ruhusa ya kufikiri hasa njia bora ya kufupisha; hana haja ya kujibidiisha mno kulichunguza lile jambo lenyewe.
32Basi, sasa tuanze masimulizi yetu; hayo tuliyoyasema yatosha kwa dibaji. Maana ni ujinga kutumia maneno mengi katika dibaji ya kitabu cha historia, na kisha kuifupisha historia yenyewe!