The chat will start when you send the first message.
1Tupa chakula chako juu ya maji;[#Kum 15:10; Mit 11:18; Mt 10:42; 2 Kor 9:6]
Maana utakiona baada ya siku nyingi.
2Uwagawie sehemu watu saba, hata wanane;[#Zab 112:9; Lk 6:30; Mik 5:5; Efe 5:16]
Maana hujui baa gani litakalokuwa juu ya nchi.
3Mawingu yakiwa yamejaa mvua,
Yataimimina juu ya nchi;
Na mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini,
Paangukapo ule mti, papo hapo utalala.
4Mwenye kuuangalia upepo hatapanda;
Naye ayatazamaye mawingu hatavuna.
5Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadhalika huijui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote.[#Yn 3:8]
6Asubuhi panda mbegu zako,
Wala jioni usiulegeze mkono wako.
Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa, kama ni hii au hii, au kama zote zitafaa sawasawa.
7Kweli nuru ni tamu, tena ni jambo la kupendeza macho kutazama jua.
8Naam, mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie yote; lakini na azikumbuke siku zijazo za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Mambo yote yajayo ni ubatili.
9Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na kinachotamaniwa na macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.[#Kum 29:19; Zab 81:12; Mdo 14:16; Efe 2:2,3; Mhu 12:14; Rum 2:6]
10Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia.[#2 Kor 7:1]