Hosea 1

Hosea 1

1Hili ndilo neno la BWANA lililomjia Hosea, mwana wa Beeri, siku za Uzia, na Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli.[#2 Pet 1:21; 2 Fal 14:23-29; 15:1-7,32-38; 16:1-20; 18:1—20:21; 2 Nya 26:1—27:8; 28:1—32:33]

Familia ya Hosea

2Hapo kwanza BWANA aliponena kwa kinywa cha Hosea, BWANA alimwambia Hosea, Nenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha BWANA.[#Kum 31:16; Amu 2:17; Zab 73:27]

3Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto wa kiume.

4BWANA akamwambia, Mwite jina lake Yezreeli; kwa maana bado kitambo kidogo, nitaipatiliza nyumba ya Yehu damu ya Yezreeli, na kuukomesha ufalme wa nyumba ya Israeli.[#2 Fal 10:11]

5Tena itakuwa siku ile, nitauvunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli.

6Akachukua mimba tena, akazaa mtoto wa kike, BWANA akamwambia, Mwite jina lake Lo-ruhama; kwa maana sitairehemu nyumba ya Israeli tena, nisije nikawasamehe kwa njia yoyote.[#1:6 maana yake ni Asiyehurumiwa.]

7Lakini nitairehemu nyumba ya Yuda; nitawaokoa kwa BWANA, Mungu wao; wala sitawaokoa kwa upinde, wala kwa upanga, wala kwa silaha, wala kwa farasi, wala kwa wapanda farasi.

8Basi, akiisha kumwachisha Lo-ruhama kunyonya, akachukua mimba, akazaa mtoto wa kiume.

9BWANA akasema, Mwite jina lake Lo-ami; kwa maana ninyi si watu wangu, wala mimi sitakuwa Mungu wenu.[#1:9 maana yake ni ‘si watu wangu’.]

Matengenezo ya Israeli

10Tena itakuwa ya kwamba hesabu ya wana wa Israeli itafanana na mchanga wa bahari, usioweza kupimwa wala kuhesabiwa; tena itakuwa, badala ya kuambiwa, Ninyi si watu wangu, wataambiwa, Ninyi ndio wana wa Mungu aliye hai.[#Mwa 26:4; Kut 32:13; Hes 23:10; Kum 1:10; 1 Fal 3:8; 1 Nya 27:23; Yn 1:12; Rum 9:26]

11Na wana wa Yuda na wana wa Israeli watakusanyika pamoja, nao watajichagulia kiongozi mmoja, nao watakwea watoke katika nchi hii; kwa maana siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya