Hosea 7

Hosea 7

1Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwizi huvunja nyumba za watu, na kundi la magaidi hushambulia nje.

2Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu.[#Mit 5:22; Zab 90:8]

3Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao.[#Rum 1:32]

4Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuri iliyotiwa moto na mwokaji; asiyehitajika kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hadi utakapokwisha kutiwa chachu.

5Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu waliugua kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha.

6Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuri, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali.

7Wote wamepata moto kama tanuri, nao hula watawala wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi.[#2 Fal 15:10; Isa 9:13]

8Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa.[#Zab 106:35]

9Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huku na huko juu yake, naye hana habari.

10Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia BWANA, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote.

Tegemeo batili kutoka kwa mataifa

11Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru.

12Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia.[#Law 26:14]

13Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu.

14Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi.[#Ayu 35:9; Zab 78:34-37; Isa 29:13; Yer 3:10]

15Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu.

16Wao hurudi, lakini si kwake Aliye Juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya ujeuri wa ndimi zao; na kwa sababu hiyo watachekwa katika nchi ya Misri.[#Zab 73:9]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya