The chat will start when you send the first message.
1Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha.[#Amu 6:12]
2Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya baba yetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine.
3Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; nao watu mabaradhuli walikwenda na kushirikiana na Yeftha katika uvamizi wake, wakatoka kwenda pamoja naye.[#Amu 9:4; 1 Sam 22:2; 30:22-24; Ayu 30:1-10; Mdo 17:5]
4Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli.
5Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu;
6wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni.
7Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Kwa nini basi mnanijia hivi sasa wakati mkiwa katika taabu?[#Mwa 26:27]
8Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi.[#Lk 17:4; Amu 10:18; Mwa 31:50; Yer 29:23; 42:5; Mik 1:2]
9Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, “Kama mkinirejesha kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye BWANA akawatoa mbele yangu, je! Nitakuwa kiongozi wenu?”
10Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye BWANA atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako.[#Rum 1:9; 1 The 2:5]
11Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kiongozi, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya BWANA huko Mispa.[#Amu 10:17; 20:1; 1 Sam 10:17; 11:15; Mit 16:3]
12Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijia kupigana juu ya nchi yangu?
13Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha, “Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea wakitoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena kwa amani.”[#Hes 21:24; Mwa 32:22]
14Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni;
15akamwambia, Yeftha anakuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni;[#Hes 22:13-15; Kum 2:9,19; 2 Nya 20:10]
16lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walipitia katika jangwa hadi Bahari ya Shamu, na Kadeshi;[#Hes 14:25; Kum 1:40; Yos 5:6; Hes 13:26; 20:1; Kum 1:46]
17ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hangewasikiliza. Pia waliwatuma wajumbe kwa mfalme wa Moabu; wala naye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi.[#Hes 20:1,14-21]
18Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki mwa nchi ya Moabu, wakapiga kambi upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu.[#Hes 21:4; Kum 2:1-8; Hes 21:11]
19Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Tunakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu.[#Hes 21:21-24; Kum 2:26; 3:1-17; Yos 13:8-12]
20Lakini huyo Sihoni hakuwaamini Israeli ili wapite ndani ya mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, nao wakapiga kambi katika Yahasa, wakapigana na Israeli.
21BWANA, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawapiga; basi Israeli wakaimiliki hiyo nchi ya Waamori, waliokaa katika nchi hiyo.[#Hes 21:24; Kum 2:33,34]
22Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hilo jangwa hadi Yordani.
23Basi sasa yeye BWANA, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe unataka kuchukua mahali pao?
24Je! Wewe hutakitamalaki hicho ambacho huyo Kemoshi mungu wako akupa kukitamalaki? Kadhalika si sisi ndio watu wa kutamalaki vyote ambavyo BWANA, Mungu wetu ametwaa kwa manufaa yetu?[#Hes 21:29; 1 Fal 11:7; Yer 48:7; Kut 23:28,31; 34:11; Hes 33:50,54; Kum 7:16,24; Yos 3:10; 2 Nya 7:20; Zab 44:2,3; Mdo 13:19]
25Na wewe sasa, je! U mwema kuliko Balaki mwana wa Sipori, huyo mfalme wa Moabu, kwa lolote? Je! Yeye alishindana na Israeli, au kupigana nao?[#Hes 22:1-6; Kum 23:3,4; Yos 24:9; Mik 6:5]
26Wakati Israeli walipokuwa wakikaa Heshboni na miji yake, na katika Aroeri na miji yake, na katika miji hiyo yote iliyo huko kando ya Arnoni, muda wa miaka mia tatu; mbona hamkuikomboa wakati huo?[#Kum 2:36]
27Basi mimi sikukufanyia wewe dhambi, lakini wewe unanitenda uovu kwa kupigana nami; yeye BWANA, yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni.[#Mwa 18:25; Ayu 9:15; Yn 5:22,23]
28Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuusikiza ujumbe aliotumiwa na Yeftha.
29Ndipo Roho ya BWANA ikamjia Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.[#Amu 3:10]
30Naye Yeftha akamwekea BWANA nadhiri, akasema, Ikiwa utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli,[#Mwa 28:20; Hes 30:2; 1 Sam 1:11; Mhu 5:1,2]
31ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na ushindi kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha BWANA, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa.[#Law 27:2; 1 Sam 1:11]
32Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye BWANA akawaua mkononi mwake.
33Akawapiga kutoka Aroeri hadi kufikia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa pigo kuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.[#Eze 27:17]
34Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na akichezacheza; naye alikuwa ni mwanawe wa pekee; hakuwa na mwingine, wa kiume wala binti.[#Amu 10:17; Kut 15:20; 1 Sam 18:6; Zab 68:25; Yer 31:4]
35Ikawa alipomuona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwa hao wanisumbuao; kwa kuwa mimi nimemfunulia BWANA kinywa changu, nami siwezi kurudi nyuma.[#Hes 30:2; Mwa 37:29; 42:36-38; 2 Sam 13:30,31; 18:33; Ayu 1:20; Mhu 5:2-5; Zab 15:4]
36Binti yake akamwambia, Baba yangu, wewe umemfunulia BWANA kinywa chako; basi unifanyie sawasawa na hayo yaliyotoka kinywani mwako; kwa kuwa yeye BWANA amekulipia kisasi juu ya adui zako, hao wana wa Amoni.[#Hes 30:2; 2 Sam 18:19]
37Kisha akamwambia baba yake, Basi na nifanyiwe neno hili; niache peke yangu muda wa miezi miwili, ili nipate kwenda milimani, na kuombolea ubikira wangu, mimi na wenzangu.[#Mwa 30:23; Lk 1:25]
38Akamwambia, Haya, nenda. Akampeleka mbali muda wa miezi miwili; naye akaenda zake, yeye na wenziwe, akauombolea ubikira wake huko milimani.
39Basi ikawa mwisho wa hiyo miezi miwili, akarudi kwa babaye, aliyemtenda sawasawa na ile nadhiri yake aliyokuwa ameiweka; naye alikuwa hajamjua mwanamume. Kisha ikawa desturi katika Israeli,[#1 Sam 1:22]
40kwamba binti za Israeli waende mwaka baada ya mwaka ili kumkumbuka huyo mwana wa Yeftha, Mgileadi, siku nne katika mwaka.