The chat will start when you send the first message.
1Basi watu wa Israeli walikuwa wameapa huko katika Mispa, wakisema, Hapana mtu yeyote kwetu sisi atakayemwoza binti yake kumpa Benyamini.[#Amu 20:1; 1 Sam 7:5,6]
2Basi hao watu wakafika Betheli, wakaketi huko mbele ya Mungu hadi jioni, nao wakainua sauti zao na kulia sana.[#Yos 18:1; Amu 20:18,26]
3Wakasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili kuwa katika Israeli, ya kwamba hivi leo kabila moja limepunguka katika Israeli?
4Kisha kesho yake, hao watu wakaamka asubuhi na mapema, wakajenga madhabahu huko, wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.[#Mwa 8:20; 12:7; Kut 20:24,25; Amu 6:26; 1 Sam 14:35; 1 Fal 8:64; Ebr 13:10]
5Wana wa Israeli wakasema, Katika hizi kabila zote za Israeli ni ipi isiyofika katika mkutano kumkaribia BWANA? Kwa maana walikuwa wameweka kiapo kikuu kuhusu huyo asiyefika kumkaribia BWANA huko Mispa, huku wakisema, Hakika yake atauawa huyo.[#Law 27:28,29; Amu 5:23; 1 Sam 11:7; Yer 48:10]
6Nao wana wa Israeli wakahuzunika kwa ajili ya ndugu yao Benyamini, wakasema, Kabila moja imekatiliwa mbali na Israeli hivi leo.
7Tufanyeje sisi ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa tumeapa kwa BWANA ya kwamba hatutawapa binti zetu ili wawaoe?
8Basi wakasema, Ni ipi katika makabila ya Israeli ambayo haikufika mbele ya Bwana huko Mispa.[#1 Sam 11:1; 31:11; 2 Sam 2:5,6]
9Kwa maana hapo watu walipohesabiwa, hakuwapo hata mtu mmoja katika wenyeji wa Yabesh-gileadi.
10Basi mkutano walipeleka huko watu elfu kumi na mbili wa hao waliokuwa mashujaa sana, kisha wakawaamuru, wakisema, Endeni mkawapige wenyeji wa Yabesh-gileadi kwa makali ya upanga, na hata wanawake na watoto wadogo.[#Kum 13:15; Yos 7:24-26; Amu 5:23; 1 Sam 11:7]
11Na jambo mtakalotenda ni hili; mtamwangamiza kila mwanamume kabisa, na kila mwanamke ambaye amelala na mwanamume.[#Hes 31:17]
12Nao wakapata katika wenyeji wa Yabesh-gileadi wanawali mia nne, ambao hawajamjua mwanamume kwa kulala naye; basi wakawaleta kambini huko Shilo, ulioko katika nchi ya Kanaani.[#Yos 18:1; 22:9; 1 Sam 1:3; Zab 78:59,60; Yer 7:12,14]
13Basi mkutano ukatuma watu na kunena na wana wa Benyamini waliokuwako huko katika jabali la Rimoni, wakawatangazia amani.[#Amu 20:47; Kum 20:10]
14Basi Benyamini wakarudi wakati huo; kisha wakawapa wale wanawake waliowasalimisha katika hao wanawake wa Yabesh-gileadi; lakini wanawake hao hawakuwatosha.
15Nao watu wakawahurumia Wabenyamini, kwa sababu BWANA alikuwa amefanya pengo katika hayo makabila ya Israeli.
16Ndipo hao wazee wa huo mkutano wakasema, Je! Tufanyeje ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa wanawake wameangamizwa katika Benyamini?
17Wakasema, Lazima uwepo urithi kwa hao wa Benyamini waliopona, lisije likafutika kabila Israeli.
18Lakini sisi hatuwezi kuwaoza binti zetu kwa maana wana wa Israeli walikuwa wameapa, wakisema, Na alaaniwe huyo atakayempa Benyamini mke.[#Amu 11:35]
19Kisha wakasema, Angalieni, iko sikukuu ya BWANA mwaka baada ya mwaka katika Shilo, mji ulio upande wa kaskazini mwa Betheli, upande wa mashariki mwa hiyo njia kuu iendeayo kutoka Betheli kwenda Shekemu, nao ni upande wa kusini mwa Lebona.
20Basi wakawaagiza hao wana wa Benyamini wakisema, Haya, endeni, mkaotee katika mashamba ya mizabibu,
21kaeni macho; kisha tazameni, kisha hao binti za Shilo watakapotoka ili wacheze katika hiyo michezo, basi tokeni mizabibuni, na kila mtu na ajishikie mke katika hao binti za Shilo, kisha mrudi katika nchi ya Benyamini.[#Kut 15:20; 32:6,19; Amu 11:34; 1 Sam 18:6; 21:11; 29:5; Yer 31:4,13]
22Kisha baba zao au ndugu zao watakapokuja kushitaki, sisi tutawaambia, Kwa hisani yenu tupeni sisi; kwa kuwa hatukumtwalia kila mtu mkewe katika vita; na kwa kuwa hamkuwapa wao, la sivyo ninyi sasa mngekuwa na hatia.
23Wana wa Benyamini wakafanya hivyo, wakajitwalia wake, kulingana na hesabu yao, katika hao waliocheza, wakawachukua wakaenda nao; kisha wakaenda kuurudia urithi wao, na kuijenga miji na kuishi humo.[#Amu 20:48]
24Nao wana wa Israeli wakati huo wakaenda zao, kila mtu akaenda kwa kabila yake na kwa jamaa yake; nao wakatoka huko, waende kila mtu kuuendea urithi wake.
25Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe.[#Amu 17:6; 18:1; 19:1; Kum 12:8; Omb 5:14; Rum 13:3-5]