The chat will start when you send the first message.
1Basi haya ndiyo mataifa ambao BWANA aliwaacha, ili awajaribu Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kanaani;[#Mwa 22:1; Kum 8:2,16; 13:3; Yn 2:24; 1 Kor 11:19]
2ili kwamba vizazi vya wana wa Israeli wapate kujua ili kuwafundisha vita, hasa wao ambao hawakujua vita kabla ya wakati ule;
3aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti, na Wakanaani wote, na Wasidoni, na Wahivi waliokaa katika kilima cha Lebanoni, toka mlima wa Baal-hermoni mpaka kuingia Hamathi.[#Yos 13:3]
4Naye aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao, apate kujua kwamba watasikiliza amri za BWANA, alizowaamuru baba zao, kwa mkono wa Musa.
5Basi wana wa Israeli wakaketi kati ya Wakanaani; hao Wahiti, na hao Waamori, na hao Waperizi, na hao Wahivi na hao Wayebusi;[#Zab 106:35]
6wakawaoa binti zao, na binti zao wenyewe wakawaoza wana wao waume, na kuitumikia miungu yao.[#Kut 34:16; Kum 7:3; Ezr 9:11]
7Wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakamsahau BWANA, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi.[#Amu 2:11; Kut 34:13; Kum 16:21; Amu 6:25]
8Kwa hiyo hasira za BWANA ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane.[#Hab 3:7]
9Kisha wana wa Israeli walipomlilia BWANA, BWANA akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.[#Amu 6:7; 10:10; 1 Sam 12:10; Neh 9:27; Zab 22:5; 106:44; Amu 2:13,16]
10Roho ya BWANA ikamjia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kuenda vitani, naye BWANA akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.[#Hes 11:17; 27:18; 1 Sam 10:6; 11:6; 16:13; 2 Nya 15:1; Ebr 6:4]
11Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arubaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.
12Basi wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu tena mbele za BWANA; naye BWANA akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli, kwa sababu walikuwa wameyafanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA.[#Amu 2:19; Yer 16:12; Hos 6:4; Mt 23:32; 1 Sam 12:9]
13Huyo Egloni akakutanisha kwake wana wa Amoni na Amaleki; akaenda na kuwapiga Israeli, nao wakauchukua huo mji wa mitende.[#Amu 5:14; Kum 34:3; Amu 1:16]
14Wana wa Israeli walimtumikia Egloni mfalme wa Moabu muda wa miaka kumi na minane.[#Law 26:23-25; Kum 28:40]
15Lakini wana wa Israeli walipomlilia BWANA, BWANA akawainulia mwokozi, Ehudi, mwana wa Gera, Mbenyamini, mtu aliyekuwa mwenye shoto; nao wana wa Israeli walimpelekea Egloni mfalme wa Moabu tunu mkononi mwa huyo Ehudi.[#Zab 50:15; 78:34; Yer 29:12,13; Dan 9:3; Amu 20:16]
16Ehudi alijifanyia upanga uliokuwa na makali kuwili, urefu wake ulipata dhiraa moja; akaufunga huo upanga ndani ya nguo yake katika paja lake la mkono wa kulia.
17Kisha akamsogezea Egloni, mfalme wa Moabu, hiyo tunu; basi Egloni alikuwa ni mtu aliyenenepa sana.
18Naye hapo alipomaliza kuitoa hiyo tunu, akawapa ruhusa watu hao walioichukua tunu, wakaenda zao.
19Lakini yeye mwenyewe akageuka kutoka huko kwenye sanamu zilizokuwa karibu na Gilgali, akasema, Mimi nina ujumbe wa siri kwako wewe, Ee mfalme. Naye akasema, Nyamazeni kimya. Watu wote waliokuwa wanasimama karibu naye wakatoka na kumwacha.[#Yos 4:20]
20Basi Ehudi akamwendea; naye alikuwa anaketi peke yake katika chumba chake cha baridi. Ehudi akasema, “Nina ujumbe wako kutoka kwa Mungu”. Basi akainuka katika kiti chake.
21Ehudi akaunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kulia, akamtia tumboni mwake;
22hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma.[#3:22 Maana ya neno la Kiebrania si dhahiri.]
23Ndipo Ehudi akatoka nje barazani, akamfungia milango ya hicho chumba na kuifunga kwa ufunguo.[#3:23 Maana yake katika Kiebrania si dhahiri.]
24Basi alipokuwa amekwisha toka nje, hao watumishi wake wakaenda; wakaona, na tazama, hiyo milango ya chumba ilikuwa imefungwa kwa ufunguo; nao wakasema, Hapana budi ameenda haja ndani ya chumba cha baridi.[#3:24 Katika Kiebrania ni kufunika miguu.]
25Wakangoja hadi wakatahayari; na tazama, hakuifungua milango ya chumba; basi wakatwaa ufunguo, na kuifungua; na tazama, bwana wao alikuwa ameanguka chini, naye amekufa.
26Naye Ehudi alikimbia hapo walipokuwa wakingoja, Ehudi alitoroka kwa kupitia huko kwenye sanamu, na kukimbilia Seira.
27Ikawa, hapo alipofika akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, ndipo wana wa Israeli wakateremka pamoja naye kutoka huko milimani, naye akawatangulia.[#Amu 5:14; 6:34; 1 Sam 13:3; Yos 17:15; Amu 7:24; 17:1]
28Akawaambia, Nifuateni; kwa kuwa BWANA amewatia adui zenu, Wamoabi, mikononi mwenu. Basi wakateremka na kumfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha Wamoabi, wala hawakumwacha mtu kuvuka.[#Amu 7:9,15; 1 Sam 17:47; Yos 2:7; Amu 12:5]
29Wakati huo wakawaua Wamoabi wapatao wanaume elfu kumi, ambao wote walikuwa wenye nguvu na mashujaa, hakunusurika hata mtu mmoja.
30Basi Moabu alishindwa siku hiyo chini ya mikono ya Israeli. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka themanini.
31Tena baada ya Ehudi alikuwapo Shamgari mwana wa Anathi, aliyewaua Wafilisti watu mia sita kwa fimbo ya kuswagia ng'ombe; naye aliwaokoa Israeli.[#1 Sam 17:47,50; Amu 2:16; #3:31 Katika Kiebrania ni ‘yake huyo’.]