The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema;
2Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli,
Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao,
Mhimidini BWANA.
3Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu;
Mimi, naam mimi, nitamwimbia BWANA;
Nitamhimidi BWANA, Mungu wa Israeli.
4BWANA, ulipotoka katika Seiri,[#Kum 33:2; Zab 68:7,8; Hab 3:3-6; Isa 64:3]
Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu,
Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondosha maji,
Naam, mawingu yakadondosha maji.
5Milima ikayeyuka mbele za uso wa BWANA,[#Kut 19:18; Kum 4:11]
Naam hata Sinai ule mbele za uso wa BWANA, Mungu wa Israeli.
6Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi,[#Amu 3:31; Law 26:22; Isa 33:8; Omb 1:4; 4:18]
Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu;
Nayo misafara ilipita kwa njia za kando.
7Watawala walikoma katika Israeli, walikoma,[#Amu 4:4-6; Isa 49:23]
Hadi mimi Debora nilipoinuka,
Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli.
8Walichagua miungu mipya,[#Kum 32:16; Amu 2:12; 1 Sam 13:19,22; Amu 4:3]
Ndipo kulikuwa na vita malangoni;
Je! Ilionekana ngao au mkuki
Katika watu elfu arubaini wa Israeli?
9Moyo wangu unawaelekea makamanda wa Israeli,
Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu;
Mhimidini BWANA.
10Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe,[#Amu 12:14]
Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani,
Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu.
11Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji,
Hapo watatangaza matendo ya haki ya BWANA;
Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli.
Ndipo watu wa BWANA waliposhuka malangoni.
12Amka, amka, Debora;
Amka, amka, imba wimbo.
Inuka, Baraka, wachukue mateka wao
Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu.
13Ndipo waliteremka mabaki ya waungwana na ya watu;
BWANA alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa.
14Kutoka Efraimu waliteremka wao ambao shina lao ni katika Amaleki,[#Amu 3:27; 4:5,6; Hes 32:39; Mwa 49:21]
Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako.
Kutoka Makiri walishuka makamanda,
Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi.
15Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora.
Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka.
Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake.
Kwenye vijito vya Reubeni
Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
16Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo,[#Hes 32:1]
Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi?
Kwenye vijito vya Reubeni
Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
17Gileadi alikaa ng'ambo ya Yordani,[#Yos 13:25; 19:29]
Na Dani, mbona alikaa katika merikebu?
Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari,
Alikaa katika hori zake.
18Zabuloni ndio watu waliohatarisha roho zao hadi kufa;[#Amu 4:10]
Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni.
19Wafalme walikuja wakafanya vita,[#Amu 4:16; Zab 44:12]
Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita.
Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido;
Hawakupata faida yoyote ya fedha.
20Walipigana kutoka mbinguni,[#Yos 10:11; Amu 4:15]
Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera.
21Mto ule wa Kishoni uliwachukua,[#Amu 4:7]
Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni.
Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu.
22Kisha, kwa kishindo kwato za farasi zilipigapiga,
Kwa maana walivyoenda shoti,
Walipowakimbiza farasi wenye nguvu.
23Ulaanini Merozi, alisema malaika wa BWANA,[#Amu 21:9; Neh 3:5; 1 Sam 17:47]
Walaanini kwa uchungu wenyeji wake;
Kwa maana hawakuja kumsaidia BWANA,
Kumsaidia BWANA juu ya hao wenye nguvu.
24Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote;[#Mit 31:31; Lk 1:28]
Mkewe Heberi, Mkeni,
Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani.
25Aliomba maji, naye akampa maziwa.
Akamletea siagi katika sahani ya heshima.
26Akanyosha mkono wake akashika kigingi,
Nao mkono wake wa kulia ukashika nyundo ya fundi;
Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake.
Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake.
27Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala.
Miguuni pake aliinama, akaanguka.
Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa.
28Alichungulia dirishani, akalia,
Mama yake Sisera alilia dirishani;
Mbona gari lake linakawia kufika?
Mbona gurudumu za gari lake zinakawia?
29Mabibi wake wenye akili wakamjibu,
Naam, alijipa jawabu.
30Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya,[#Kut 15:9]
Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu?
Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbalimbali,
Nyara za mavazi ya rangi mbalimbali ya darizi;
Ya rangi mbalimbali ya darizi, pande zote mbili,
Juu ya shingo za hao mateka.
31Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee BWANA.[#Zab 48:4,5; 58:11; Ufu 6:10; 18:20; 2 Sam 23:4; Zab 37:6; Mt 13:43; Zab 19:5]
Bali wao wampendao na wawe kama jua hapo litokapo kwa nguvu zake. Nayo nchi ikastarehe miaka arubaini.