The chat will start when you send the first message.
1Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka asubuhi na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni.[#Amu 6:32; 1 Sam 12:11; Mwa 22:3; Yos 3:1; 6:12; Mhu 9:10; Mwa 12:6]
2BWANA akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno kwangu kuwatia Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa.[#Kum 8:17; 9:4; 32:27; 1 Sam 17:47; Zab 33:16-18; 44:6,7; Mit 25:6; Mhu 9:11; Isa 10:13; Yer 9:23,24; Zek 4:6; Rum 3:27; 1 Kor 1:29; 4:7; 2 Kor 4:7; 10:17; Efe 2:9]
3Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu yeyote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu elfu ishirini na mbili wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi.[#Kum 20:8]
4BWANA akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; walete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda.[#1 Sam 16:6,7]
5Basi akawaleta watu chini majini. BWANA akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa.
6Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji.
7BWANA akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake.[#1 Sam 14:6; Isa 41:14,18]
8Basi Gideoni akachukua vyakula vyao na tarumbeta zao, kisha akawaaga watu wote wa Israeli, kila mtu hemani mwake; akabaki na watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni.[#7:8 Katika Kiebrania ni ‘wale watu’.]
9Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako.[#Mwa 46:2,3; Ayu 4:13; Mt 1:20; Mdo 18:9,10; 27:23]
10Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini;
11nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya, mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hadi katika vituo vya walinda zamu wa kambi ya Wamidiani.[#Mwa 24:14; 1 Sam 14:9,10]
12Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia wao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi.[#Amu 6:5,33; 8:10]
13Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, niliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika katika hema moja, ukaipiga hadi ikaanguka, ukaipindua, hadi ikalala chini.[#Amu 6:15; Isa 41:14,15; 1 Kor 1:27]
14Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake.[#Mwa 40:8; Hes 23:5]
15Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana BWANA amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu.
16Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo na maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi.[#Hes 10:9; Yos 6:4; 2 Nya 13:14,15; Amo 3:6]
17Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni vivyo hivyo.
18Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa BWANA, na kwa Gideoni.
19Basi Gideoni, na wale watu mia moja waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao.[#Kut 14:24; Lk 12:38; Ufu 16:15]
20Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kulia ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa BWANA na wa Gideoni.
21Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza.[#Kut 14:13,14,25; 2 Nya 20:17; Isa 30:7,15; 2 Fal 7:7; Ayu 15:21,22; Mit 28:1]
22Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye BWANA akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuelekea Serera, hadi mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi.[#Yos 6:4,16,20; 2 Kor 4:7; 1 Sam 14:20; Zab 83:9; Isa 9:4; 19:2; 2 Nya 20:23]
23Wanaume wa Israeli walikuwa wamekusanyika kutoka Naftali, na kutoka Asheri, na kutoka Manase yote, wakawafuata Midiani.
24Kisha Gideoni akatuma wajumbe katika nchi yote ya vilima vilima ya Efraimu, akisema, Haya, teremkeni juu ya Midiani, na kuyatwaa hayo maji mbele yao, mpaka Bethbara, maana huo mto wa Yordani. Basi wanaume wote wa Efraimu walitokeza wakayatwaa maji mpaka Bethbara, yaani, huo mto wa Yordani.[#Amu 3:27; Rum 15:30; Flp 1:27; Amu 3:28; Yn 1:28]
25Wakawashika hao wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu; wakamwua huyo Orebu pale penye jabali la Orebu, na huyo Zeebu wakamwua hapo penye shinikizo la divai la Zeebu, kisha wakawaandamia Wamidiani; vichwa vya Orebu na Zeebu wakamletea Gideoni huko ng'ambo ya pili ya Yordani.[#Amu 8:3,4; Zab 83:11; Isa 10:26]