Yoshua 13

Yoshua 13

Sehemu za Kanaani ambazo hazijatekwa

1Basi Yoshua alipokuwa mzee, na miaka yake kwendelea sana, BWANA akamwambia, Wewe umekuwa mzee na miaka yako kwendelea sana, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa.[#Mwa 18:11; Yos 14:10; 24:29; 1 Fal 1:1; Lk 1:7]

2Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote;[#Kut 23:29,31; Kum 11:23,24; Amu 3:1; Mwa 10:14; 26:1; Yoe 3:4; 1 Sam 27:8; 2 Sam 3:3]

3kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; watawala watano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi,[#Yer 2:18; 1 Sam 6:4,16; Sef 2:5; Kum 2:23]

4upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori;[#Yos 19:30; Amu 1:34; #13:4 matoleo mengine ‘Ara’.]

5na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa mashariki ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikia maingilio ya Hamathi;[#1 Fal 5:18; Zab 83:7; Eze 27:9; Yos 12:7]

6na watu wote wenye kukaa nchi za vilima kutoka Lebanoni hadi Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru.[#Hes 33:54; Yos 11:8; 23:13; Amu 2:21; Yos 14:1,2]

7Basi sasa gawanya nchi hii, iwe urithi wa hizi kabila tisa, na nusu ya kabila la Manase.

Nchi iliyo mashariki mwa Yordani

8Pamoja na yeye, Wareubeni na Wagadi walipata urithi wao, waliopewa na Musa, huko ng'ambo ya Yordani upande wa mashariki, vile vile kama huyo Musa mtumishi wa BWANA alivyowapa;[#Hes 32:33; Kum 3:12; Yos 22:4; #13:8 au nusu ile nyingine ya kabila la Manase.]

9kutoka huko Aroeri, iliyoko pale ukingoni mwa bonde la Amoni, na huo mji ulioko pale katikati ya bonde, na nchi tambarare yote ya Medeba mpaka Diboni;[#Hes 21:30; Isa 15:2; Yer 48:18,22]

10na miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni, hata mpaka wa wana wa Amoni;

11na Gileadi na mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka, na mlima wa Hermoni wote, na Bashani yote mpaka Saleka;[#Yos 12:5]

12ufalme wote wa Ogu uliokuwa katika Bashani, huyo aliyekuwa akitawala katika Ashtarothi na katika Edrei (huyo alisalia katika mabaki ya wale Warefai); kwa kuwa Musa aliwapiga hao na kuwafukuza.[#Kum 3:11; Hes 21:24]

13Pamoja na hayo wana wa Israeli hawakuwafukuza Wageshuri, wala Wamaaka; lakini Wageshuri na Wamaaka wamekaa kati ya Israeli, hadi siku hii ya leo.

14Lakini hakuwapa watu wa kabila la Lawi urithi wowote ule; maana sadaka za BWANA, Mungu wa Israeli, zisongezwazo kwa njia ya moto ndizo urithi wake huyo, kama alivyomwambia.[#Kum 18:1; 10:9; 12:12,19; Hes 18:20; Yos 14:3,4]

Nchi ya Reubeni

15Musa akawapa kabila la wana wa Reubeni kwa kadiri ya jamaa zao.

16Mpaka wao ulikuwa kutoka hapo Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Arnoni, na huo mji ulio katikati ya bonde, na nchi tambarare yote iliyo karibu na Medeba;[#Hes 21:28,30; Kum 3:12; Yos 12:2]

17na Heshboni na miji yake yote iliyoko katika bonde; na Diboni, na Bamoth-baali, na Beth-baal-meoni;

18na Yahasa, na Kedemothi, na Mefaathi;[#Hes 21:23]

19na Kiriathaimu, na Sibma, na Sereth-shahari katika kilima cha hilo bonde;[#Hes 32:37]

20na Beth-peori, na nchi za materemko ya Pisga, na Beth-yeshimothi;

21na miji yote ya nchi tambarare, na ufalme wote wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akitawala katika Heshboni, aliyepigwa na Musa pamoja na hao wakubwa wa Midiani, nao ni Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao watawala wa Sihoni, waliokuwa katika nchi hiyo.[#Kum 3:10; Hes 21:24; 31:8]

22Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.[#Hes 22:5; 24:1; 31:8; 2 Pet 2:15; Ufu 2:14]

23Na mpaka wa wana wa Reubeni ulikuwa ni mto wa Yordani, na kingo zake. Huo ndio urithi wa wana wa Reubeni sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake.

Nchi ya Gadi

24Musa akawapa kabila la Gadi, hao wana wa Gadi, kwa kadiri ya jamaa zao.

25Mpaka wao ulikuwa ni Yazeri, na miji hiyo ya Gileadi, na nusu ya nchi ya wana wa Amoni, mpaka Aroeri uliokabili Raba;[#Hes 32:35; 21:26-29; Kum 2:19; Amu 11:13; 2 Sam 11:1; 12:26]

26tena kutoka Heshboni mpaka Ramath-Mizpe, na Betonimu; tena kutoka Mahanaimu hadi mpaka wa Debiri;

27tena katika bonde, Beth-haramu, na Bethnimira, na Sukothi, na Safoni, hiyo iliyosalia ya ufalme wa Sihoni mfalme wa Heshboni, yaani mto wa Yordani na kingo zake, mpaka mwisho wa bahari ya Kinerethi ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki.[#Mwa 33:17; 1 Fal 7:46; Hes 34:11; Kum 3:17; Yos 11:2; Mt 14:34; Lk 5:1]

28Huo ndio urithi wa wana wa Gadi sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake.

Nchi ya nusu kabila la Manase (mashariki)

29Kisha Musa akawapa hao wa nusu ya kabila la Manase urithi wao; ulikuwa ni wa hiyo nusu ya kabila la wana wa Manase sawasawa na jamaa zao.

30Na mpaka wao ulikuwa kutoka huko Mahanaimu, Bashani yote, na ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, na miji yote ya Yairi, iliyo katika Bashani, miji sitini;[#Hes 32:41; 1 Nya 2:23]

31na nusu ya Gileadi, na Ashtarothi, na Edrei, hiyo miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani, ilikuwa ni ya wana wa Makiri mwana wa Manase maana, kwa hiyo nusu ya wana wa Makiri sawasawa na jamaa zao.[#Yos 12:4]

32Hizi ndizo mirathi ambazo Musa alizigawanya katika nchi tambarare za Moabu, ng'ambo ya pili ya Yordani, kukabili Yeriko, upande wa mashariki.

33Lakini Musa hakuwapa kabila la Lawi urithi uwao wote; yeye BWANA, Mungu wa Israeli, ndiye urithi wao, kama alivyowaambia.[#Hes 18:20; Yos 18:7; Kum 10:9; 12:12; 14:27,29; 18:1,2; Eze 44:28]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya