The chat will start when you send the first message.
1Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao wakatoka Shitimu, wakafika katika mto wa Yordani, yeye na wana wa Israeli wote, wakakaa hapo kabla ya kuvuka.[#Hes 25:1; 33:49; Yos 2:1]
2Ikawa baada ya siku tatu, viongozi wakapita katikati ya kambi,[#Yos 1:10,11]
3wakawaamuru watu wote wakisema, Mtakapoliona sanduku la Agano la BWANA, Mungu wenu, na makuhani Walawi wakilichukua, ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata.[#Hes 10:33; Kum 31:9]
4Lakini, na iwe nafasi kati ya ninyi na lile sanduku, kama dhiraa elfu mbili kiasi chake; msilikaribie mpate kuijua njia ambayo hamna budi kuiendea; kwa maana hamjapita njia hii bado.[#Kut 19:12; Kum 28:58; 1 Nya 16:30; Zab 2:11; 96:9; Ebr 12:28]
5Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho BWANA atatenda mambo ya ajabu kati yenu.[#Kut 10:10; Law 20:7; Hes 11:18; Yos 7:13; 1 Sam 16:5; Yoe 2:16]
6Kisha Yoshua akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la Agano, mkavuke mbele ya hao watu. Wakaliinua sanduku la Agano, wakatangulia mbele ya watu.[#Hes 4:15]
7BWANA akamwambia Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya kuwa mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa.[#Yos 4:14; 1 Nya 29:25; 2 Nya 1:1]
8Nawe uwaamuru hao makuhani walichukuao sanduku la Agano, ukawaambie, Mtakapofika ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani.
9Basi Yoshua akawaambia wana wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya BWANA, Mungu wenu.
10Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa kuwatoa mbele yenu Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi.[#Kum 5:26; 1 Sam 17:26; 2 Fal 19:4; Hos 1:10; Mt 16:16; 1 The 1:9; Kut 33:2; Kum 7:1; Zab 44:2]
11Tazama, sanduku la Agano la Bwana wa dunia yote linavuka mbele yenu na kuingia Yordani.[#Zab 24:1; Ayu 41:11; Mik 4:13; Zek 4:14; 6:5]
12Basi sasa twaeni watu kumi na wawili katika makabila ya Israeli, kila kabila mtu mmoja.[#Yos 4:2]
13Itakuwa, wakati nyayo za makuhani walichukuao sanduku la BWANA, Bwana wa dunia yote, zitakaposimama katika maji ya Yordani, hayo maji ya Yordani yataacha kutiririka, maji yale yashukayo kutoka juu; nayo yatasimama kama kichuguu.[#Kut 15:8; Zab 78:13; 114:3; Hab 3:15]
14Hata ikawa, hao watu walipotoka katika hema zao, ili kuvuka Yordani, makuhani waliolichukua sanduku la Agano wakatangulia mbele ya watu,[#Kut 25:10; 26:30; Hes 10:3; 2 Nya 6:41; Zab 132:8; Mdo 7:45; Ebr 9:4]
15basi hao waliolichukua hilo sanduku walipofika Yordani, na nyayo za makuhani waliolichukua sanduku zilipotiwa katika maji ya ukingoni, (maana Yordani hujaa hata kingo zake na kufurika wakati wote wa mavuno),[#1 Nya 12:15; Yer 12:5; 49:19; Yos 4:18; 5:10,12]
16ndipo hayo maji yaliyoshuka kutoka juu yakasimama, yakainuka, yakawa kichuguu, mbali sana, huko Adamu, mji ule ulio karibu na Sarethani, na maji yale yaliyoteremkia bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yataacha kutiririka kabisa; watu wakavuka kukabili Yeriko.[#1 Fal 4:12; 7:46; Kum 3:17; Mwa 14:3; Hes 34:3]
17Na hao makuhani waliolichukua sanduku la Agano la BWANA wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Yordani; Israeli wote wakavuka katika nchi kavu, hadi taifa lile lote likaisha kuvuka Yordani.[#Kut 14:29; Ebr 11:29]