Yoshua 4

Yoshua 4

Mawe kumi na mawili yasimamishwa pale Gilgali

1Ikawa, hapo hilo taifa zima lilipokuwa limekwisha vuka Yordani, ndipo BWANA akanena na Yoshua, akamwambia,[#Kum 27:2; Yos 3:17]

2Haya, twaeni watu wanaume kumi na wawili katika hao watu, kila kabila mtu mmoja,[#Hes 13:2; 34:18; Kum 1:23; Yos 1:4-15; 3:12; 1 Fal 18:31]

3kisha uwaamrishe, kusema, Twaeni mawe kumi na mawili, hapo katikati ya Yordani, mahali hapo miguu ya hao makuhani iliposimama imara, mwende na mawe hayo, mkayaweke mahali pale kambini ambapo mtalala usiku huu.

4Basi Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili, aliokuwa ameteua tangu hapo awali, katika wana wa Israeli, kila kabila mtu mmoja;

5naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la BWANA, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mmoja wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya makabila ya wana wa Israeli;

6ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya?[#Kut 12:26; 13:14; Kum 6:20; Zab 44:1; 78:3-6; Isa 38:16]

7Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yaliondoka mbele ya sanduku la Agano la BWANA; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalisimama; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele.[#Yos 3:13; Kut 12:14; Hes 16:40; 1 Kor 11:24]

8Basi wana wa Israeli walifanya vile vile kama Yoshua alivyowaamuru, nao wakatwaa mawe kumi na mawili pale katikati ya Yordani, kama BWANA alivyomwambia Yoshua, sawasawa na hesabu ya makabila ya wana wa Israeli; wakayachukua wakavuka nayo hata mahali pale walipolala, nao wakayarundika huko.

9Kisha Yoshua akapanga mawe kumi na mawili katikati ya Yordani, mahali pale miguu ya hao makuhani waliolichukua hilo sanduku la Agano iliposimama; nayo yapo pale pale hata hivi leo.[#Mwa 28:18; Yos 24:27; 1 Sam 7:12]

10Kwa kuwa makuhani waliolichukua hilo sanduku walisimama katikati ya Yordani, hadi mambo yote BWANA aliyomwamuru Yoshua awambie hao watu yakaisha, sawasawa na hayo yote Musa aliyokuwa amemwamuru Yoshua; kisha hao watu wakafanya haraka wakavuka.

11Ikawa watu wote walipokuwa wamekwisha vuka kabisa, hilo sanduku la BWANA likavuka, na hao makuhani, mbele ya macho ya hao watu.

12Na wana wa Reubeni, na wana wa Gadi na hiyo nusu ya kabila la Manase, wakavuka, wakiwa wamebeba silaha mbele ya wana wa Israeli, kama Musa alivyowaambia;[#Hes 32:20]

13walikuwa kama watu elfu arubaini waliobeba silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya BWANA, waende vitani, hadi nchi tambarare za Yeriko.

14Siku ile BWANA alimtukuza Yoshua mbele ya macho ya Israeli wote; nao wakamcha, kama walivyokuwa wakimcha Musa, siku zote za maisha yake.[#Yos 3:7; 1 Sam 2:30; 1 Nya 29:12,25; 2 Nya 1:1; 32:23]

15Kisha BWANA akanena na Yoshua, akamwambia,

16Haya, uwaamuru makuhani, hao waliolichukua sanduku la ushuhuda, kwamba wakwee juu kutoka mle katika Yordani.[#Kut 25:16; Ufu 11:19; Yos 3:15]

17Basi Yoshua akawaamuru hao makuhani, akawaambia, Haya, kweeni mtoke Yordani.

18Ilikuwa, hapo hao makuhani waliolichukua sanduku la Agano la BWANA walipokwea juu kutoka mle kati ya Yordani, na nyayo za miguu yao hao makuhani zilipoinuliwa na kutiwa katika nchi kavu, ndipo maji ya Yordani yaliporudi mahali pake, na kufurika katika kingo zake zote, kama yalivyokuwa hapo kwanza.

19Na hao watu wakakwea kutoka Yordani siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi Gilgali, katika mpaka wa mashariki wa Yeriko.[#Yos 5:9; 15:7; 1 Sam 11:14,15; Amo 4:4; 5:5; Mik 6:5]

20Na yale mawe kumi na mawili waliyoyatwaa katikati ya Yordani Yoshua akayasimamisha Gilgali.

21Akawaambia wana wa Israeli, akasema, Watoto wenu watakapowauliza baba zao katika siku zijazo, wakisema, Mawe haya maana yake ni nini?

22Ndipo mtakapowaarifu watoto wenu mkisema, Israeli walivuka mto huu wa Yordani, kwa njia ya nchi kavu.

23Kwa sababu BWANA, Mungu wenu aliyakausha maji ya Yordani, mbele yenu, hadi mlipokwisha kuvuka kama BWANA, Mungu wenu, alivyoitenda Bahari ya Shamu, aliyoikausha mbele yetu hata tulipokwisha kuvuka;[#Kut 14:21; Neh 9:11; Zab 77:16,19; 78:13; Isa 43:16; 63:12]

24watu wote wa duniani wapate kujua mkono wa BWANA, ya kuwa ni mkono wenye uweza, na ili nanyi mpate kumcha BWANA, Mungu wenu, milele.[#Kut 9:16; Kum 28:10; 1 Sam 17:46; 1 Fal 8:42; 2 Fal 5:15; 19:19; Zab 89:7; 106:8; Yer 32:40; Dan 3:26-29; Kut 15:16; 1 Nya 29:12; Kut 14:31; Kum 6:2; Zab 76:6-8; Yer 10:7]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya