The chat will start when you send the first message.
1Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, majusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema,[#Lk 2:1-7]
2Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.[#Hes 24:17]
3Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.
4Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi?
5Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Yudea; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii,[#Mik 5:2; Yn 7:42]
6Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,[#Mik 5:1]
Hu mdogo kamwe miongoni mwa watawala wa Yuda;
Kwa kuwa kwako atatoka mtawala
Atakayewachunga watu wangu Israeli.
7Kisha Herode akawaita wale majusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota.
8Akawatuma Bethlehemu, akasema, Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.
9Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, mpaka iliposimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto.
10Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno.
11Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu, uvumba na manemane.[#Zab 72:10,15; Isa 60:6]
12Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.
13Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hadi nitakapokuambia; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.[#Kut 2:15]
14Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;
15akakaa huko hadi Herode alipokufa; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema,[#Hos 11:1]
Kutoka Misri nilimwita mwanangu.
16Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale majusi, alighadhibika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wa kiume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake kote, kuanzia wenye miaka miwili na chini yake, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale majusi.
17Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema,[#Yer 31:15]
18Sauti ilisikiwa Rama,[#Yer 31:15; Mwa 35:19]
Kilio na maombolezo mengi,
Raheli akiwalilia watoto wake,
Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawapo tena.
19Herode alipofariki, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri,
20akasema, Inuka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto.[#Kut 4:19]
21Akainuka akamchukua mtoto na mamaye, akaenda katika nchi ya Israeli.
22Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anatawala huko Yudea mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda pande za Galilaya,
23akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazareti.[#Mk 1:24; Lk 1:26; 2:39; Yn 1:45; Isa 11:1; 53:2]